Polisi nchini Norway sasa wanasema kuwa mtu aliyekuwa na bunduki aliyefyatua risasi katika mkusanyiko wa vijana katika kisiwa yenye kambi ya vijana nje ya mji mkuu, Oslo, Ijumaa jioni aliuwa watu wasiopungua 80.
Hatimaye mtu huyo alikamatwa kwenye kisiwa hicho, na polisi wanamhusisha piya na mripuko wa bomu katika jumba la ofisi za serikali katika mji mkuu, ambao uliuwa watu wengine 7.
Kulipopambazuka leo asubuhi ndio maafa hayo yalionekana wazi katika kisiwa cha Utoeya.
Baada ya kuthibitisha awali kuwa watu 10 tu waliuwawa, polisi mara walitangaza kuwa watu kama 80 wamekufa.
Mshambuliaji aliyekuwa na bunduki, aliyejifanya kuwa askari polisi, aliwashambulia wanachama wa tawi la vijana la chama tawala cha Labour.
Vijana mamia kadha walikuwa wamejumuika katika kisiwa hicho katika kambi ya likizo, wengi walikuwa matineja.
Anita Bakaas alieleza jinsi binti yake alivojificha chooni wakati akimsikia mshambuliaji akimpiga risasi kijana mmoja nje ya choo.
Walionusurika wanaeleza jinsi baadhi ya marafiki zao walijitupa kati ya wale waliouwawa, wakitaraji mshambuliaji hatotambua, lakini aliwapiga risasi wote waliolala chini kwa kuwalenga mmoja-mmoja kwa bunduki.
Waziri wa Mashauri ya Nchi za Nje wa Norway, Jonas Storr, alisema watu wa Norway wako katika mshtuko mkubwa.
Mshambuliaji huyo mwenye umri wa miaka 32, sasa ameshtakiwa kwa mashambulio yote mawili.
Vyombo vya habari vya Norway vimemtaja kuwa Anders Behring Breivik, na inaarifiwa amewahi kueleza maoni makali ya kifashisti.
0 Comments