SERIKALI imesema ubadilishaji wa leseni za udereva sasa itakuwa mpaka Desemba 31 mwaka huu na kuagiza wamiliki na madereva wa mabasi yote ya abiria kuweka namba za simu kwenye mabasi yao.
Pia katika mwaka 2011/2012 Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa itawapatia vitambulisho wafanyakazi wa Serikali, wanafunzi wa vyuo na vyuo vikuu katika awamu ya kwanza, ambapo mradi huo utakapokamilika utagharimu kiasi cha Sh bilioni 355.
Akiwasilisha hotuba ya Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi kwa mwaka 2011/2012, bungeni jana, Waziri Shamsi Vuai Nahodha ambaye anaomba Bunge limuidhinishie matumizi ya fedha Sh bilioni 482.3, alisema idadi ya makosa barabarani imeongezeka kwa asilimia 7.1
Alisema, katika kipindi cha Januari hadi Desemba mwaka jana, makosa ya usalama barabarani 384,676 yaliripotiwa katika vituo vya Polisi hali hiyo ni tofauti ukilinganisha na makosa 359,305 ya kipindi cha Januari na Desemba 2009.
Wizara imekusudia kupunguza ajali za barabarani kwa asilimia 10 kwa mwaka 2011/2012 kwa kuwa asilimia 75 ya ajali hizo zinasababishwa na makosa ya kibinadamu ikiwemo uzembe, ulevi na mwendo kasi.
“Jeshi la Polisi limekuwa likiwahimiza wamiliki wa mabasi ya abiria yanayokwenda mikoani kufunga mitambo ya kutoa taarifa za mwendo (car tracking), kuwataka madereva kuendesha kwa mwendo wa usalama na kukata leseni mpya.
“Nimeliagiza Jeshi la Polisi lisisite kuwanyang’anya leseni madereva wazembe na wanaosababisha ajali, vilevile nimeliagiza jeshi hilo kuwataka wamiliki na madereva wa mabasi ya abiria waweke namba za simu kwenye mabasi yao ili abiria watoe taarifa za uzembe unaofanywa na madereva kwa Polisi,” alisema.
Alisema, Polisi kwa kushirikiana na Mamlaka ya Mapato (TRA) walianza kutoa leseni za elektroniki awamu ya kwanza katika vituo mbalimbali nchini na kuwa hadi Mei 24 mwaka huu leseni 105,518 zilitolewa kwa madaraja mbalimbali.
0 Comments