Sakata la Diwani wa Kata ya Nzovwe kupitia Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Hezron Mwakarobo kutangazwa kujiuzulu wadhifa wake na kuhamia Chama cha Mapinduzi (CCM) limeingia sura mpya baada ya Meya wa Jiji la Mbeya, Athanas Kapunga kusisitiza kuwa Mwakarobo sio tena diwani na ni mwanachama halali wa CCM.
Kapunga alisema hatua ya Mwakarobo kuandika barua ya kujiuzulu wadhifa wake wa udiwani, ilikuwa ni hitimisho tu la mchakato wa kujiunga na CCM.
Kapunga alisema kabla ya kujiuzulu kwake, Mwakarobo alimwendea na kumweleza nia yake ya kujiuzulu na kujiunga na CCM na hivyo yeye (Kapunga), kama kiongozi wa CCM, aliamua kumchukua diwani huyo na kumkabidhi kwa Katibu wa CCM mkoa wa Mbeya, Verena Shimbusho.
Alisema Mwakarobo alikabidhi kadi yake ya Chadema yenye namba D 2009005150 kwa katibu huyo na likabakia suala moja tu la kumkabidhi kadi mpya ya CCM, ambayo ilipangwa kuwa akabidhiwe na Nape Nnauye kwenye mkutano wa CCM uliofanyika mwishoni mwa juma.
Kapunga pia alionyesha baadhi ya picha zilizopigwa zikimwonyesha Mwakarobo akiwa katika ofisi ya Katibu wa CCM mkoa wa Mbeya, akimkabidhi Shumbusho kadi yake ya Chadema.
Alisema baada ya hatua hiyo kukamilika, Julai 11, mwaka huu Mwakarobo aliwasilisha barua ya kujiuzulu udiwani ambayo aliikabidhi katika ofisi ya Mkurugenzi wa Jiji la Mbeya na nakala yake kuituma katika ofisi ya Meya wa Jiji kwa taarifa.
Kapunga alisema baada ya kuipata barua hiyo, Julai 12, mwaka huu alitekeleza wajibu wake wa kisheria kwa kumjulisha Waziri mwenye dhamana ya Serikali za mitaa, Mkuu wa Mkoa wa Mbeya na Mkuu wa Wilaya ya Mbeya.
Alisema Julai 12, mwaka huu Mkurugenzi wa Jiji naye alitoa taarifa ya kujiuzulu kwa diwani huyo katika ofisi ya Katibu Mkuu Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, Katibu Tawala wa Mkoa wa Mbeya na kwa Mkuu wa Wilaya ya Mbeya.
Alisema Julai 13, mwaka huu alipokea barua nyingine kutoka kwa Mwakarobo ikifuta tamko lake la kujiuzulu.
Kufuatia tamko hilo la Meya alilolitoa mbele ya Kaimu Mkurugenzi wa Jiji la Mbeya James Jorojik, Diwani wa kata ya Mabatini na Mwenyekiti wa Kamati ya Halmashauri ya Jiji la Mbeya inayoghushulikia Mipangomiji na Mazingira, Patrick Makwalu na Diwani wa Kata ya Nonde Godian Mwambasa, Kata ya Nzovwe ambayo alikuwa akiiongoza Mwakarobo imetangazwa kuwa ipo wazi.
Katibu wa Chadema Mkoa wa Mbeya, Eddo Mwamalala, alidai msimamo wa chama chake ni kwamba Mwakarobo bado ni diwani halali wa kata ya Nzovwe kupitia Chadema.
Jumamosi iliyopita, Katibu wa CCM mkoa wa Mbeya, Verena Shumbusho, alitangaza kwenye mkutano wa CCM Jijini Mbeya kuwa Mwakarobo ni miongoni mwa wanachama 497 wa Chadema waliohamia CCM na ambao wangekabidhiwa kadi na mgeni rasmi wa mkutano huo, Nnauye.
Hata hivyo, Mwakarobo hakujitokeza mkutanoni kukabidhiwa kadi ya CCM na badala yake juzi aliibuka na kukanusha v kuhamia CCM.
CHANZO: NIPASHE