Mnenguaji wa siku nyingi wa bendi ya Twanga Pepeta, Aisha Madinda, amejiunga na bendi ya Extra Bongo 'Next Level' ambayo iko chini ya ukurugenzi wa Ally Choki.
Aisha alitambulishwa na Choki jana mbele ya waandishi wa habari katika ukumbi wa Mzalendo Pub, Makumbusho, jijini Dar es Salaam
Katika utambulisho huo, Choki, alisema kuwa ana uhakika mnenguaji huyo atatoa mchango mkubwa katika bendi yake, kwa madai kwamba ni mzoefu wa kazi na pia ana mashabiki wengi.
"Wapo baadhi ya watu wamekuwa wakidai kuwa Aisha amechoka, lakini ukweli ni kwamba bado ana uwezo mkubwa wa kufanya kazi kama alivyo Banzastone ambaye naye alianza kubezwa," alisema Choki.
Choki alisema kuwa mnenguaji huyo atatambulishwa rasmi kwenye bendi hiyo kesho Jumatano katika onyesho litakalofanyika ndani ya ukumbi wa Masai uliopo Ilala.
Alifafanua kuwa utambulisho wa Aisha utaendelea Ijumaa wiki hii ambapo bendi hiyo itakuwa mjini Musoma mkoani Mara ikifanya vitu vyake katika ukumbi wa Magereza.
Aliongeza kuwa Jumamosi Extra Bongo itakuwa jijini Mwanza na kisha Jumapili itamalizia burudani na kumtambulisha mnenguaji huyo kwenye mikoa ya Kanda ya Ziwa Victoria mjini Geita.
"Nina uhakika nguvu imeongezeka kwenye shoo ya Extra Bongo hasa kwa kuzingatia kwamba uwezo wa Aisha ninaujua kutokana na ukweli kwamba nilishafanya naye kazi kwa muda mrefu," alisema.
Kwa upande wake, Aisha, alisema kuwa ameachana na Twanga Pepeta baada ya kuona watu wake ambao alikuwa akifanya nao kazi kwa karibu wamehamia Extra Bongo.
"Kule kwa sasa hakuna vitu kama ambavyo viko Extra Bongo, hivyo ninawaomba mashabiki wangu waje huku Extra Bongo wanione nikiendeleza makamuzi kwani bado niko fiti katika muziki," alisema Aisha.
Alisema kuwa wiki moja iliyopita alikuwa kwenye mazoezi makali chini ya kiongozi wa shoo wa Extra Bongo, Super Nyamwela ili kuzijua staili za bendi hiyo na kwamba sasa yuko tayari kupanda jukwaani na kufanya vitu vyake.
CHANZO: NIPASHE
0 Comments