Sasa inajulikana kuwa watu karibu 100 wamekufa katika mashambulio ya bunduki na bomu nchini Norway siku ya Ijumaa
Watu wa Norway wanakusanyika kuwakumbuka waliokufa kwenye mashambulio.

Polisi wanasema mtu waliyemshtaki kwa mashambulio yote mawili, Anders Behring Breivik, amewaambia kuwa alifanya hayo peke yake.

Wanasema hawamsaki mtu yoyote mwengine.

Wakili wa Anders Behring Breivik anasema mteja wake amekiri kuwa alifanya mashambulio yote mawili na yuko tayari kujieleza mahakamani.

Uchunguzi unaendelea mwahala mwa mashambulio hayo - kambi katika kisiwa cha Utoya, na barabara kati ya mji wa Oslo ambapo bomu lilotegwa kwenye gari liliripuka.



Inajulikana kuwa, kwa uchache, watu 85 walikufa katika kisiwa cha Utoya, na kama 7 mjini Oslo.

Manuwari ndogo zinatumiwa kutafuta watu ambao pengine walizama walipokuwa wakijaribu kukimbia mauaji katika kisiwa cha Utoya.

Wakati uchunguzi unaendelea, watu katika sehemu mbali mbali za Norway wanakusanyika kuomboleza baada ya lile liloelezewa kuwa shambulio kubwa kabisa nchini humo tangu Vita vya Pili vya Dunia.

Watu wamekesha katika kanisa kuu la Oslo, watu wanasali na bendera zinapepea nusu mlingoti.

Baadhi ya watu wamelalamika juu ya namna polisi walivoshughulikia mashambulio hayo.

Na habari zaidi zinaibuka kuhusu mshtakiwa Anders Behring Breivik.

Aliweka video yake kwenye YouTube, ikimuonesha analenga bunduki ya rashasha.

Piya inasemekana alitoa maelezo kwenye mtandao wa internet, akilaani Uislamu kuingia bara la Ulaya.