Polisi wanne wamefikishwa mbele ya mahakama moja nchini Nigeria kuhusu mauwaji ya kiongozi wa wanamgambo wa Kiislamu Mohammed Yusuf mwaka 2009.
Kiongozi wa kikundi hicho cha Boko Haram alikamatwa akiwa hai huko Maiduguri na kuonekana katika picha za video lakini baadae maiti yake ilionekana ikiwa imeshambuliwa kwa risasi.

Kesi hiyo ilianza mapema mwaka huu lakini kwa siri haikuwa wazi kwa umma. Kumekuwa na mfululizo wa mashambulio yanayokihusisha kikundi hicho. Mengi ya mashambulio hayo huwalenga polisi.
Kwa mujibu wa mwandishi wa BBC Habiba Adamu ambaye alikuwa mahakamani, kumekuwa na ulinzi mkali nje na ndani ya mahakama hiyo ya Abuja wakati kesi hiyo ilipoanza kusikizwa.
Kesi hiyo kwa sasa imeahirishwa hadi jumanne ijayo wakati polisi wa tano atajumuishwa katika kesi hiyo na mashtaka rasmi kuwasilishwa dhidi yao.
Serikali ya Nigeria mara kwa mara imekuwa ikishutumiwa kwa kukosa kuwaadhibu polisi wanaoshutumiwa kwa ukatili na mauwaji kinyume na sheria.

Mapigano kuleta utawala wa Kiislamu


Miaka miwili iliyopita vikosi vya usalama vya Nigeria vilizima kwa ukatili ghasia za Boko Haram na kushambulia makao yao makuu na vile vile kumkamata Bw Yusuf.
Badala ya kutoeka, kikundi hicho kinachopinga elimu ya kimagharibi na azma yake ya kuanzisha utawala wa Kiislamu limeibuka tena mwezi September na kuapa kulipiza kifo cha kiongozi wao.
Mwezi uliopita, kikundi hicho kilisema kimeshambulia makao makuu ya polisi wa Nigeria mjini Abuja, mashambulio yaliosababisha vifo vya watu 6.
Mashambulio mengi hufanyika katika mji wa kaskazini mashariki wa Maiduguri katika jimbo la Borno ambako maelfu ya watu wamekimbia makwao katika siku za hivi majuzi.
Siku ya jumanne chuo kikuu cha Maiduguri kilifungwa kutokana na ukosefu wa usalama.
Vikosi vya usalama pia vimeshutumiwa kwa kufyatua risasi kiholela na kusababisha mauwaji ya raia wakati vinapofanya mashambulio yake.