Wasema samaki hao si salama
  
Kule walikataliwa, wakaletwa TZ
  
Madhara yaainishwa kitaalam
  
Chiba na Fukushima ni km 220.43
Sakata la kuingizwa kwa samaki wanaohofiwa kuwa na mionzi ya sumu ya nyukilia limechukua sura mpya, baada ya raia wa Tanzania wanaoishi nchini Japan kuitahadharisha Serikali kuwa waangalifu na majibu yatakayotolewa kutoka kwenye samaki hao kwa manufaa ya Watanzania.
Wakiongea kwa masharti ya kutoandikwa majina yao, Watanzania hao walisema onyo lao linatokana na kufahamu mazingira ya samaki hao walivyopatikana na njia zilizotumika hadi kutua nchini humu.
Walisema kugundulika kwa kuingizwa kwa samaki hao nchini, kumetokana na juhudi zao baada ya kugundua kuna shehena kubwa ya samaki waliokataliwa nchini humo zinasafirishwa kwenda Tanzania.
Walisema kuingizwa kwa makontena matano ilikuwa kama njia moja ya kujaribu kama hawatatiliwa wasiwasi kabla ya kuanza kuingizwa kwa samaki wengi kutoka nchini Japan.
Wametahadharisha mji wa Chiba ambao samaki hao wanasadikiwa kutoka na mji wa Fukushima ulioathirika na mionzi ya nyuklia ni kilomita 220.43 tu sawa na umbali wa kutoka Dar es Salaam na Morogoro.
“Serikali isipokuwa na tahadhari itawaangamiza wananchi wake wenyewe, naomba umakini uwepo wa majibu yao ama sivyo wengi wataangamia,” alisema mmoja wa raia hao wanaoishi nchini Japan.
Hata hivyo, alisema kitendo cha kupelekwa makontena ya samaki kutoka Japan kwenda Tanzania walitilia shaka na kuamua kuwapa taarifa wenzao ili angalau suala hilo liwe wazi.
“Sio makontena hayo matano tu yaliyofika nyumbani, kuna samaki wengi ambao walikuwa katika mpango wa kuletwa endapo suala hili lisingebainika mapema, alisema.
Wasiwasi wa wananchi hao umeungwa mkono na baadhi wa wakazi wa jijini, ambapo wameitaka serikali kusikiliza hofu za Watanzania na waache kuangalia maslahi ya watu binafsi.
Hemed Makungu mkazi wa Mtoni alisema hata kazi ya kuchunguza sakata hilo kupewa Mamlaka ya Chakula na Dawa (TFDA) ilikuwa makosa makubwa hasa ukizingatia chombo hicho kimehusika kutoa kibali cha kuingizwa kwa samaki hao.

Alisema Serikali inatakiwa uchunguzi huu ungefanywa na chombo kingine huru ili kuepuka mchezo mchafu kutofanyika katika kupata majibu.
“Toka lini mtu aliyefanya kosa akapewa nafasi ya kujihukumu, hapa wanatupiga changa la macho tu kinachotakiwa chombo huru kitumike kupata ukweli,” alisema Makungu.
Hata hivyo, Serikali jana ilitoa tamko la kuwapeleka samaki hao nje ya nchi kwa ajili ya kuwafanyia vipimo baada ya majibu ya vipimo vilivyotolewa na Tume ya mionzi nchini kuonyesha samaki hao hawana madhara kwa binadamu.
Waziri wa Maendeleo ya mifugo na Uvuvi, David Mathayo, alisema serikali imechukua hatua hiyo ili kujiridhisha ili waweze kuchukua hatua sahihi juu ya samaki hao.
“Tunataka kuhakikisha kama kweli yaliyosemwa na tume yetu ya nguvu ya Atomiki imesema kweli, kama ni kweli hawana mionzi tutaruhusu samaki kuendelea kuuzwa,” alisema Mathayo.
UTAFITI WA KITAALAMU UNASEMAJE?
Urenium inayorutubishwa ni mchananganyiko wa madini ya Protoni, madini joto (Aodin) na Neuton ambazo kwa kawaida huwa zinazotoa mnunurusho wa Isotop (Atomiki).
Kutokana na mchanganyiko huo, Nyuklia hii inapowekwa sehemu maalum na kusindikwa zina nguvu kubwa za kutengeneza nguvu ya umeme.
Kwa kawaida Isotop zinazotokana na Urenium za kurutubishwa zinakuwa sio imara na zinapovuja zinameguka haraka pale zinapopaa angani au kuanguka chini.
Kwa kawaida Isotop za Atomiki hizi kutokana na kutokuwa na uimara zinapokwenda angani au chini zinameguka ambapo kitendo cha kumeguka hutoa mnunurisho (mionzi).
Kitendo cha kumeguka kwa Isotop za nyuklia zinatoa mnunurusho ambao una mwanga kama wa radi na zina nguvu za kuchoma kama mashine ya kuchomea vyuma.
WATU WANAPATAJE ATOMI ZA ISOTOP ZA NYUKLIA
Mara nyuklia inapovuja kutoka kwenye kinu, hutoa mvuke uliojaa Isotop ambazo nyingi huelea angani na zingine huangukia ardhini na kwenye maji.
Zinapoangukia kwenye maji, chembechembe hizi hukimbilia kwa haraka katika mimea iliyo kwenye maji pamoja na kumezwa na samaki wakati wakinywa maji.
Lakini samaki hao wanapokula majani hayo kama chakula chao huongeza idadi ya Isotop za nyuklia ndani ya mwili wake na huendelea kuongeza kiwango kwa kula majani na samaki wengine.
Ndani ya samaki hawa, kitendo cha kumeguka kinaendelea na kusababisha samaki kupoteza nguvu zake za asili.
Pia Chembechembe hizi zinaweza kuwepo ndani ya mboga mboga na majani na endapo binadamu au mnyama yoyote atakula majani hayo atakuwa amepatwa na chembechembe hizo.
Hivyo chemchembe hizi za Atomi zinapokuwa ndani ya viumbe hai au angani zitakuwa zinaendelea kumeguka na kutoa mnunurisho.
ATOMI ZINAVYOATHIRI CHEMBECHEMBE HAI ZA BINADAMU.
Mnunurisho (mionzi) wa Atomi unapokuwa ndani ya mwili wa binadamu unakuwa na nguvu kama mashine ya kuchomea vyuma, hivyo ni rahisi kuunguza chembechembe hai ndani ya mwili.
Kwa kawaida chembechembe hai za binadamu ni teketeke na pale zinapokutana na mionzi ya Atomi zinaweza kusambaratishwa haraka.
Pia DNA ambazo zina kazi ya kutengeneza chembechembe hizo nazo zinapokutana na mionzi huwa zinakatwakatwa na kushindwa kutengeneza chembechembe hai.
Kibaya zaidi mionzi hii ya Atomi inapoingia ndani ya mwili wa binadamu hukimbilia katika maeneo ambayo kuna DNA zinazozalisha chembechembe hai kwa haraka kama mdomoni, tumboni, utumbo, ute uliopo ndani ya mifupa (uboho), rovu (koromeo) koradani kwa wanaume na kwenye via vya uzazi kwa wanawake.
Atomi hizi zinapokuwa ndani ya mwili na kuendelea kumeguka, mnunurisho wake unazuia uzaliaji wa chembechembe hai na kuvuruga mpangilio mzima wa mifumo ya hewa, chakula na uzazi. Tunaweza kusema kwa urahisi mionzi hii ya Atomi inafanya kazi kama virusi vinapoingia ndani ya kompyuta na kuvuruga mfumo wake.
DALILI ZA MTU ALIYEPATWA NA MIONZI.
Kama mtu amepata dozi kubwa ya mionzi ya nyuklia anapata dalili zifuatazo.
1.Kupatwa na kichefuchefu, kutapika na wakati mwingine hutapika damu.
2.Mwili unadhoofika.
3.Anavuja damu kila mahali.
4.Anaharisha mfululizo
5.Anapungukiwa na kinga za mwili.
6.Anapatwa na saratani kutokana na mvurugano wa DNA kwenye mwili.
7.Kwa mwanamke anaweza kuharibu mimba au kiumbe kutoka kikiwa na mapungufu ya viungo.Aidha mtoto anayezaliwa anaweza kuwa na saratani au akawa mgumba kutokana na kuwa na mionzi mwilini mwake.
8. Anapungukiwa na damu kutokana na uboho kutoweza kutengeneza chembechembe hai nyekundu.
KUJIKINGA KAMA IKITOKEA.
Kitaalamu inaelezwa endapo kinu cha nyuklia kinapovuja au kuwepo na sababu zingine zinazosababisha kuenea kwa nyuklia, inapaswa kujikinga kama ifuatavyo.
1. Endapo kutatokea na athari hizo ni vyema watu wakapewa madini joto kwa wingi ili kusababisha madini joto yanayotokana na Urenium yasiweze kutoa mionzi inayoleta madhara kwa watu.
2. Kuvaa mavazi imara yasiyoweza kuruhusu mionzi au mvuke wa Atomi za Asotipu kuingia mwilini.
3. Kuvaa vifaa maalum kwenye pua na mdomo (Maski) ili kuzuia kuvuta hewa iliyojaa Atomi za Isotop.
4. Inashauriwa watu kutokula chakula, mbogamboga au maji na mazao yanayotokana kwenye maji yaliyochafuliwa na Atomi.
Maelezo haya ni kwa msaada wa wataalamu na mtandao.
CHANZO: NIPASHE JUMAPILI