ASKARI 21, wameuawa katika kipindi cha mwaka 2005 mpaka sasa wakati wakitekeleza majukumu yao ya kikazi, hatua inayoonesha kuwa polisi wanafanya kazi katika mazingira magumu na hivyo Jeshi la Polisi kuamua kueneza kampeni ya umuhimu wa utii wa sheria bila shuruti kwa wananchi.

Hayo yalisemwa na Mkuu wa Operesheni wa Jeshi la Polisi, Kamishna Paul Chagonja, wilayani Karagwe mkoani Kagera wakati wa mazishi ya askari namba EX F.4268 D/C Pendo aliyeuawa na jambazi Tarime wakati alipokuwa akitekeleza majukumu yake ya kikazi ambapo askari huyo ndiye anayetimiza idadi ya askari 21.


Kamishna Chagonja alisema, pamoja na vifo hivyo bado askari hawatarudi nyuma katika kupambana na uhalifu kwa kuwa wamekula kiapo kwa kazi hiyo na watatumia nguvu zao zote kukabiliana na wahalifu wakataokuwa wanahatarisha maisha ya raia na mali zao.



Alisema, huu ni wakati muafaka kwa wananchi kuitumia kampeni ya utii bila shuruti kwa kuwa jamii nzima ikiwa adilifu matumizi ya nguvu hayatakuwepo na taifa litasonga mbele katika uchumi.


Mkuu wa Wilaya ya Karagwe, Kanali mstaafu Fabian Massawe akitoa salamu za rambirambi, alisema jamii haina budi kushirikiana na Jeshi la Polisi katika kuwabaini na kuwafichua wahalifu ili waweze kufikishwa katika vyombo vya sheria.


Kanali Massawe alitoa mwito kwa wakazi wa Karagwe kutii agizo lililotolewa na Jeshi la Polisi la kusalimisha silaha ambazo zinamilikiwa isivyo halali kuanzia Agosti Mosi 2011 hadi Oktoba 2011 ili mkono wa sheria usije ukawakumba.


Kwa upande wake baba mzazi wa marehemu, Jovini Pendo aliwataka vijana wengine kutokata tamaa ya kujiunga na Jeshi la Polisi kwa kuwa kilichotokea ni ajali kama ajali nyingine.


Alisema, anajivunia mtoto wake kwa kuwa alikuwa akifanya kazi ya kuilinda nchi hivyo hata askari wengine waliobakia hawana budi kuwa imara katika kupambana na uhalifu kama alivyokuwa akifanya mtoto wake.


Mazishi hayo pia yalihudhuriwa na Kamati nzima ya Ulinzi na Usalama ya Wilaya ya Karagwe, Makamanda wa Polisi wa Mikoa ya Kagera na Mkoa wa Kipolisi wa Tarime/Rorya, askari na wananchi wa kijiji cha Igurwa.