Wakimbizi wa Kisomali katika kambi ya Dadaab
Mkuu wa shirika la kuwashughulikia wakimbizi duniani anatarajiwa kuwasilisha ombi kwa serikali ya Kenya kutoa kambi mpya kwa waathirika wanaokimbia ukame katika upembe mwa Afrika.
Antonio Guterres anakutana na rais Mwai Kibaki wa Kenya mjini Nairobi ambapo ataomba kibali cha kumaliza ujenzi wa kambi mpya itayayowapa makaazi wakimbizi 80,000.
Hata hivyo wenyeji kulikojengwa kambi za wakimbizi wa Kisomali wamepinga mpango huo wakisisitiza kwamba huenda raia hao wakazifanya makaazi yao ya kudumu.
Licha ya changamoto zilizoko, Antonio Guterres ameipongeza serikali ya Kenya kwa kuwapokea maelfu ya wakimbizi wa Kisomali wanaokimbia ukame na kuingia katika kambi ya Dadaab kaskazini mwa nchi.
Lakini mazingira katika kambi hiyo yametajwa kama ya kusikitisha kutokana na idadi kubwa ya wakimbizi waliosongamana. Hali hii ndiyo imepelekea Bw. Guterres kuomba kikao maalum na rais Kibaki kumshawishi ampe kibali kumaliza ujenzi wa kambi mpya ambayo ujenzi wake ulianza mwaka jana.
Kambi hiyo inatarajiwa kuwapa hifadhi wakimbizi 80,000, wanaokimbia vita na ukame nchini Somalia. Kambi hiyo ambayo inanuia kuwa na maji safi na umeme ilisimamishwa mwaka jana baada ya serikali kupinga ujenzi wake.
Raia wa Kenya wanaoishi eneo hilo wameonekana kutounga mkono upanuzi wa kambi za wakimbizi. Japo wanaridhia kuwasaidia wenzao waliokimbia vita, hofu yao ni kwamba wakimbizi wa Kisomali watafanya kambi hizo makao yao ya kudumu.
0 Comments