RAIA wa kigeni wa Ethiopia 22 wamehukumia kifungo cha miaka mitatu jela na kulipa faini ya shilingi laki moja kila mtu katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Mkoa baada ya kupatikana na hatia ya kuingia nchini bila kibali.

Hukumu hiyo ilitolewa jana na hakimu mkazi Zabibu Mpangule baada ya kuridhika na maelezo yaliyotolewa na upande wa jamhuri.

Awali, wakisomewa maelezo ya kosa na mwendesha mashtaka wakili wa serikali Epafras Njau mbele ya Hakimu mkazi Mpangule alidai kuwa washitakiwa hao kwa pamoja walikamatwa na Askari wa uhamiaji Juni 28 katika maeneo ya Kaloleni mji mdogo wa Tunduma mkoani hapa.

Raia hao wa kigeni walihukumiwa kifungo hicho ni Mohamed Shano (18), Ally Abdulrahman (18), Safi Hassan (22), Kadire Hassan (25), Sultan Haji (20), Kamar Subi (30), Abdisa Kabato (18), Musa Bami (21), Anah Kadir (18), Abdukadir Kadir (25).

Wengine ni Khalid Kassim (18), Tucha Shule (17), Hamza Hassan (18), Abdukadir Hussein (16), Abal Angule (17), Burhan Kimo (28), Yasin Kassim (20), Tebabu Mikone (20), Abdumalik Mohammed (35), Adamu Shika (17) na Abdallahy Gari (18).

Mpangule alisema anatoa adhabu hiyo ili iwe fundisho kwa raia wengine wanaoingia nchini bila kibali.