Msimamo huo ulionyeshwa jana na Balozi wa Marekani nchini, Alfonso Lenhardt, alipotembelea kituo cha Tomondo Sober House, kinachotoa huduma kwa vijana walioachana na utumiaji wa dawa za kulevya katika eneo la Tomondo, mjini hapa.
“Uamuzi wenu wa kijiunga na vituo hivi ni njia sahihi zaidi katika vita vya kupambana na biashara ya dawa za kulevya duniani, kwa sababu hatimaye biashara hiyo itakosa soko,” alisema Balozi Lenhardt.
Alisema ameelezwa kuwa zaidi ya vijana 300 walioachana na dawa za kulevya wamepitia katika kituo cha Tomondo Sober House na kupatiwa huduma mbali mbali na kwamba asilimia 30 kati yao sio mateja tena baada ya kurejea katika maisha ya kawaida.
Tomondo Sober Haouse ni miongoni mwa vituo vitano vinavyotoa huduma ya aina mbali mbali, ikiwemo elimu kwa vijana walioamua kuachana na matumizi ya dawa za kulevya katika visiwa vya Unguja na Pemba.
Akifafanua msimamo wa Marekani katika vita dhidi ya biashara ya dawa za kulevya, Balozi Lenhardt, alisema nchi yake ina amini njia sahihi ya kufanikisha vita hiyo ni kuua soko lake kwa watumiaji kuacha kuyatumia.
“Tunahitaji vijana zaidi kama ninyi, wanaume na wanawake, kujitokeza kuachana na dawa za kulevya, sisi kama nchi tutasaidia kuwaelimisha wasitumie dawa hizo, mkifanikiwa kutotumia, wauzaji pia wataacha kuzileta Zanzibar,” alisema Balozi Lenhardt.
0 Comments