Machafuko yamezuka mji mkuu wa Malawi, Lilongwe, wakati makundi ya upinzani yakipinga serikali ya Rais Bingu wa Mutharika(pichani juu).
Mwandishi wa BBC mjini Lolongwe Joel Nkhoma, amesema waandamanaji walikuwa wanachoma vizuizi barabarani na kupora.
Serikali imezuia radio kutangaza moja kwa moja ghasia hizo.
Matatizo yalianza baada ya mahakama kutoa hukumu siku ya Jumanne kwamba maandamano ya nchi nzima, yaliyoitishwa kupinga kupanda gharama za maisha, ni haramu.

Mwandishi wa BBC amesema licha ya uamuzi huo wa mahakama, maandamano pia yamefanyika katika mji mkuu wa kibiashara Blantyre, na katika mji wa kaskazini wa Mzuzu.
Lakini hali imekuwa mbaya zaidi mjini Lilongwe, ambapo waandamanaji wenye hasira walikuwa wakipiga kelele, "Mutharika aondoke", amesema mwandishi wetu.


Mwandishi huyo amesema polisi walifyatua mabomu ya kutoa machozi na wameweka vizuizi barabarani kuzuia waandamanaji kuingia katikati ya mji wa Lilongwe, ambapo maduka yote yamefungwa na mitaani hakuna watu.

Kwa mujibu wa mwandishi wetu ghasia zipo zaidi katika miji midogo iliyo karibu na Lilongwe ya Biwi, Kawale na Nchesi.

Kumekuwa na majibizano ya kushambuliana kati ya polisi na waandamaji, kwa mujibu wa msemaji wa Tume ya Haki za Binadamu ya Malawi Mike Chipalasa.

"Watu wana hasira sana. Hali si nzuri hapa," amesema.

Duka linalomilikiwa na Mbunge kutoka chama kinachotawala cha Democratic Progressive Party (DPP) na ghala la mfanyabiashara mwenye uhusiano na Rais Mutharika yameporwa kwa mujibu wa mwandishi wa BBC.

Pia kuna taarifa za kuchomwa moto nyumba za askari polisi watatu mjini Lilongwe.

Polisi pia wamezuia kamera ya mpiga picha mmoja aliyekuwa akipiga picha maandamano hayo.

Kuna taarifa nyingine zinasema polisi walimpiga risasi sikioni mwandamanaji mmoja, wakati mali ya waziri mmoja iliposhambuliwa.

Maandamano hayo yaliitishwa kupinga kupanda bei ya mafuta, upungufu wa hazina ya fedha za kigeni, kukosekana utawala bora na uhusiano mbaya wa kimataifa.

Wiki iliyopita Uingereza ilisimamisha misaada kwa Malawi baada ya kutokea mzozo wa kidiplomaisa na serikali ya Mutharika.

Uingereza iliishutumu Malawi kwa kushindwa kusimamia uchumi na haki za binadamu.

Hivi karibuni serikali ilipitisha hatua za kubana matumizi, ikapandisha kodi na kupunguza utegemezi wa misaada.

Malawi ni moja ya zilizo masikini sana duniani, ikikadiriwa asilimia 75 ya watu wa nchi hiyo wanaishi chini ya dola moja kwa siku