Mawaziri Wakuu Wastaafu, Jaji Joseph Sinde Warioba (kushoto) na Dkt Salim Ahmed Salimu(kulia) wakisikiliza kwa makini hotuba ya ukaribisho kutoka kwa Mkuu wa Chuo cha Kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere Dkt John Magotti(hayupo pichani) wakati wa uzinduzi wa maadhimisho ya miaka 50 ya uanzishwaji wa Chuo hicho.(Picha na Tiganya Vicent- Maelezo Dar es Salaam).

WAZIRI Mkuu mstaafu, Jaji Joseph Warioba amekemea malumbano yanayoendelea kutokea bungeni kwa sasa, akisisitiza kuwa chombo hicho ni kioo cha wananchi hivyo kina wajibu wa kuendesha mambo yake kwa nidhamu na kwa uadilifu mkubwa.

Warioba aliyasema hayo jana jijini Dar es salaam wakati akitoa mada katika ufunguzi wa maadhimisho ya miaka 50 ya Chuo cha Kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere ambayo kilele chake itakuwa ni Desemba 5, mwaka huu.



Alisema: “Hali ya malumbano inanyemelea Bunge, lugha isiyo staha inaanza kutawala majadiliano ndani na nje ya Bunge, vituko, kejeli, vijembe na kelele zisizo na nidhamu vinaanza kuwa tabia ndani ya bunge… mara nyingi hoja nzito zinaazimwa kwa vituko na matumizi mabaya ya kanuni na taratibu,” alisema na kuongeza:


“Kuna utetezi kwamba mabunge kwenye nchi zenye demokrasia ya vyama vingi ni kawaida wabunge kutumia lugha ya kubeza, kejeli vituko hata kupigana lakini sio jambo jema kuiga mambo ambayo hayana tija ila tunapaswa kuiga mambo yanayoambatana na utamaduni wetu au yatakayotufaa.


Alisisitiza: “Kama lugha ya wabunge imejaa kejeli na kubeza wananchi nao wataiga, kama wabunge watasema milango ifungwe watwangane na wananchi wataona kutwangana ni njia ya kumaliza mjadala”.


Aidha, Warioba alisema nchi ipo katika hali ya dharura ya kipindi kigumu kutokana na tatizo kubwa la nishati, chakula na bei ya mafuta hivyo ni wakati wa viongozi hasa wa vyama vya siasa kuungana na kutoa suluhisho la pamoja badala ya kufanya kampeni zisizo na mwisho.


Alisema; “matatizo makubwa yanayowakabili wananchi hayapewi uzito unaostahili, hivi sasa, nchi inapita katika kipindi kigumu, hali ya chakula ni wasiwasi, kuna njaa kali katika nchi jirani na bei ya shilingi inashuka hivyo ni wakati wa kushughulikia matatizo haya ya dharura kwa pamoja”.


Pia Warioba alisema kuwa malumbano kati ya vyama vya siasa limekuwa ni jambo la kawaida na wamejikita zaidi kwenye kashfa ambapo kwa sasa imekuwa ni jambo la kawaida kwa viongozi kushtakiana kwa wananchi kwenye mikutano na maandamano.


“Ninavyoona mimi tumeanza kupuuza baadhi ya misingi yetu na nidhamu yetu kama taifa imeshuka kwa kutozingatia muda kwa viongozi na wananchi,” alisema.


Alisema viongozi waliopita katika chuo hicho ambacho zamani kilijulikana kama Kivukoni walijifunza misingi ya malengo ya Taifa, itikadi na sera za Taifa, nidhamu, maadili na wajibu wa viongozi kama kundi katika utumishi wa umma na kiongozi mmoja mmoja mahali alipo.

Aliongeza kuwa kutokana na hilo nchi iliweza kupata uongozi wenye mwelekeo mmoja siyo tu kwa nadharia bali kwa vitendo.

Alisema kuwa maadili ya taifa yamepuuzwa ambapo baadhi ya viongozi wamekuwa wakizungumzia sana suala la rushwa na ufisadi lakini vitendo vyao vimekuwa vikitoa picha tofauti na vinaonesha njia ya kwenda kwenye rushwa na ufisadi.


Alihoji: “Hivi ni wangapi kati yetu anaweza kusimama mbele ya muumba wake na kusema katika kutafuta uongozi hakutoa hongo? Wanatoa hongo kwa maana hongo ndiyo njia pekee inayowezesha kuchaguliwa na mgombea asiyeitoa haonekani ni kiongozi”.


Alisema kuwa viongozi wasipoonesha kwa vitendo kukataa rushwa na ufisadi itakuwa ni kazi bure na kwamba chuo hicho kilijenga mwelekeo wa kitaifa kwa kujenga uongozi ulioimarisha umoja na mshikamano wa taifa.


“Hali ya sasa imebadilika sana kuna dalili za makundi na kauli zinazotolewa na viongozi mbalimbali ndani ya serikali zinaleta wasiwasi kama kuna mwelekeo wa uwajibikahi wa pamoja, vyama vyote vya siasa vikubwa na vidogo vina matatizo hayo” alisema.


Alisema kuwa zamani kikao kikubwa cha chama cha siasa kikikutana wananchi walingojea maamuzi kwa hamu kubwa na mara nyingi maamuzi hayo yalihusu maendeleo ya wananchi lakini kwa siku hizi vikao hivyo vinapokutana wananchi wanangojea kusikia vita vya wakubwa vimefikia wapi.


Aidha alisema kuwa mgawanyo wa madaraka kati ya serikali na Bunge umeanza kuonesha mgongano ambapo pia Taasisi za utendaji kama Polisi, Takukuru na Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali ambazo zinatakiwa kufanya kazi kwa uhuru na taratibu kwa sasa zinapewa msukumo wa kisiasa.


Akichangia mada hiyo kwa uchungu huku akitokwa na machozi, mwakilishi wa Mwenyekiti wa TLP, Augustino Mrema, Getrude Pwila alisema kuwa bunge kwa sasa limepoteza mwelekeo na kuwataka wanawake waomboleze kwa ajili ya taifa lao.


Kwa upande wake Humphrey Sambo ambaye ni mwanafunzi wa chuo hicho alisema kuwa ni aibu kwa sasa mtu kukaa na kupoteza muda kuangalia bunge kwa sababu wabunge wanaongea bila mpangilio na hawaoneshi kama kweli wamepitia vyuo.


Mwakilishi kutoka taasisi ya Mwalimu Nyerere, Gallus Abeid alisema kuwa uzalendo na uadilifu ni bidhaa ambazo zimeanza kutoweka Tanzania na kutaka chuo hicho kusaidia kurudiisha maadili na uzalendo.


Pia aliwataka viongozi kuacha kuwa madalali wa kuuza ardhi ya Watanzania kwa wageni kwa kisingizio cha kuwaita wawekezaji.


Naye mgeni rasmi katika maadhimisho hayo Dk. Salim Ahmed Salim alisema kuwa wananchi bado wanathamini misingi ya maendeleo, undugu na kushikamana na kuvitaka vyama vyote kuelewa upinzani hauna maana ya kulumbana na kupingana wakati wote hata katika masuala ya maendeleo ya taifa.


Dk. Salim ambaye pia ni Mwenyekiti wa Bodi wa chuo hicho, alihitimisha kwa kusema kuwa pamoja na tofauti na matatizo yanayoikabili nchi lakini kunatakiwa kuimarisha umoja na kupigania haki kwa maslahi ya wote.