MBUNGE wa Monduli, Edward Lowassa amesema anafurahi kuanzisha mjadala unaoendelea nchini hivi sasa.
Akizungumza kwa kifupi, alisema kila mtu atakuwa na fursa ya kujipima na wananchi ndio wataamua.
Lowassa alikuwa aliyasema hayo ofisini kwake Mikocheni Dar es Salaam jana, alipokuwa akikabidhi Sh milioni 13 zilizotolewa na jamaa na marafiki zake kusaidia ujenzi wa Shule ya Sekondari ya Edward Lowassa, ya watoto yatima iliyopo Mikwabe Kigamboni Dar es Salaam.
Alitoa matamshi hayo, baada ya kuulizwa na waandishi wa habari kuhusu kauli aliyoitoa bungeni karibu wiki mbili zilizopita kuhusu haja ya serikali kutoogopa kuchukua uamuzi mgumu kuhusiana na masuala mbalimbali ya maendeleo ya nchi.


Kauli hiyo imezua mjadala kutoka kwa viongozi mbalimbali nchini.
Baadhi ya viongozi waliokwisha kuizungumzia kauli hiyo ya Lowassa ni Waziri Mkuu, Mizengo Pinda na Waziri wa Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Samuel Sitta na Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Nape Nnauye.
Akizungumza bungeni karibu wiki mbili zilizopita, Lowassa ambaye pia ni Waziri Mkuu mstaafu alisema katika miaka 50 ya Uhuru, zimewisha kuchukuliwa hatua mbalimbali za maendeleo ambazo dunia nzima inajua.
Lakini, alisema, hivi sasa serikalini imekuwapo tabia ya kuogopa kuthubutu na kuchukua uamuzi mgumu.
Lowassa ambaye alikuwa akishiriki katika mjadala wa makadirio ya matumizi ya Ofisi ya Waziri Mkuu kwa Mwaka wa Fedha 2011/12.

Kwa mujibu wa Lowassa ni bora mtu ukalaumiwa kwa kufanya uamuzi mgumu kuliko kulaumiwa kwa kutofanya uamuzi na kwamba Serikali inapaswa kufanya uamuzi bila kujali matokeo yake huku akipendekeza kwa kuanzia, ikope kwa kutumia rasilimali za nchi na kuendeleza miradi mikubwa
kama reli na bandari.
“Ni bora kulaumiwa kwa kufanya uamuzi kuliko kulaumiwa kwa kutofanya uamuzi
kabisa,”alisema Lowassa na kuongeza:”Kuna ugonjwa wa kutokutoa uamuzi hapa na lazima tukubali kubadilike. Ni heri mtu ukosee kutoa uamuzi kuliko kukaa kimya kabisa, heri uhukumiwe kwa kutoa uamuzi kuliko ulaumiwe kwa kushindwa kutoa uamuzi,”alisema.
Alitoa mfano wa mambo yanayoweza kutekelezwa kuwa ni kama vile kujenga upya reli ya kati na bandari zote nchini kwa kutumia fedha za humu humu.
Mbunge huyo alisema hata gesi ambayo ni nyingi nchini inaweza kutumika kukopea fedha kwa ajili ya utekelezaji wa miradi hiyo.
Pia akizungumza katika mahojiano na Kituo cha Televisheni ya TBC juzi, Lowassa alisema Watanzania wanafahamu na kutambua alichokisema.

Alichosema Pinda
Naye Waziri Mkuu Pinda wakati akihitimisha hotuba ya makadirio ya matumizi ya fedha ya ofisi yake alisema Serikali zote tangu uhuru zimekwisha kuchukua uamuzi mgumu wa masuala mbalimbali.
Waziri Mkuu Pinda alisema si tu Serikali hii ya awamu ya nne iliyopata kufanya uamuzi
mgumu, bali serikali zote zilizotangulia zimepata kufanya uamuzi mgumu, lakini
yakizigatia “busara na umakini”.
“Uamuzi mgumu ni sehemu ya
maisha ya Serikali katika kutekeleza majukumu yake kwa dhana ya uwajibikaji wa pamoja (collective responsibility) kupitia Baraza la Mawaziri. Tunachohitaji ni kuvumiliana, kuvuta subira, kwani mambo mema hayataki haraka. Tutaamua na tutafanya”.
Akianisha maeneo karibu 12 ambayo Serikali imepata kufanya uamuzi, Pinda
alisema: “Serikali ya awamu ya nne imekuwa ikifanya uamuzi thabiti na mgumu, lakini kwa busara na tahadhari ili kutenda haki na kwa kuzingatia uwezo wa Serikali kulinda maslahi ya wananchi kudumisha amani. Katika kufanya uamuzi huo, Serikali imekuwa makini kuzingatia sheria, kanuni na taratibu.
“Tunatambua kuwa moja ya sifa za kiongozi ni kuweza kufanya uamuzi. Tunayo historia ya viongozi ambao tunawakumbuka kwa uamuzi huo kwa taifa hili.
“Mfano mzuri, ni Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere. Wakati wa uongozi wake,moja ya uamuzi mgumu ambao aliufanya na tunaukumbuka ni kuruhusu nchi yetu kuingia katika harakati za kusaidia nchi za Bara la Afrika ambazo zilikuwa hazijapata uhuru”.
Alitaja mifano ya nchi zilizofaidika na uamuzi mgumu wa Mwalimu Nyerere kuwa ni pamoja na Angola, Afrika Kusini, Msumbiji, Namibia na Zimbabwe.
Aliongeza: “Vilevile, tunakumbuka uamuzi mgumu uliofanywa na Baba wa Taifa kuwasaidia ndugu zetu wa Uganda kujikomboa kutoka kwenye Utawala wa Dikteta Iddi Amin. Lakini pia tunakumbuka
uamuzi mzito uliofanywa na Baba wa Taifa kuhusu vita dhidi ya walanguzi, uamuzi ambao ulisababisha baadhi ya wafanyabiashara kutupa bidhaa barabarani.”
Waziri Mkuu alisema pia kwamba yapo maeneo mengi ya uamuzi mzito ambao umefanywa na uongozi wa awamu ya pili na awamu ya tatu.
Pinda alisema Serikali ya awamu ya nne imekamilisha miradi yote 27 ya barabara kuu zilizoanzishwa na Rais mstaafu, Benjamin Mkapa.
“Tumesimamia ujenzi na ukamilishaji wa miradi ya maji nchini, tumefanya uamuzi mzito katika kuwalinda watu wenye ulemavu wa ngozi na tumefanikiwa.
“Tumeondoa mpasuko wa kisiasa Zanzibar, tumefanya uamuzi mgumu ya kukubali kuanzisha Serikali ya Umoja wa Kitaifa katika Serikali ya Mapinduzi Zanzibar.
“Tumefanya uamuzi wa kupanua na kushamiri kwa demokrasia nchini kwa kiwango kikubwa.
Nadhani, hii ndilo linasababisha baadhi yetu sasa tunajisahau na kuanza kutumia uamuzi huo visivyo. Tunahamasisha maandamano huku tukijisifu kwamba huo ndiyo uzalendo.
“Tumefanya uamuzi wa kuruhusu uhuru mkubwa wa vyombo vya habari. Mtu anaandika anachotaka, na uhuru wa kusema lolote. Hivi karibuni tumefanya uamuzi wa kuruhusu kuanzisha mchakato wa kupata Katiba Mpya. Hili nalo siyo jambo dogo hata kidogo,” alisema Pinda na kuongeza;
“Lakini pia katika awamu hii ndipo tumefanya uamuzi mzito sana wa kuvunja Baraza la Mawaziri kufuatia kujiuzulu kwa aliyekuwa Waziri Mkuu, Edward Lowassa. Hili nalo halikuwa jambo jepesi hata kidogo. Inataka moyo!”

Alichosema Sitta
Wiki iliyopita akizungumza bungeni, Waziri wa Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Samuel Sitta alisema ni vigumu serikali kuweza kufanya uamuzi mgumu kama baadhi ya watu si waadilifu.
Sitta ambaye pia ni Mbunge wa Urambo Mashariki, alisema uamuzi mgumu hauwezekana ikiwa baadhi ya watu wanashiriki katika kufanya mikataba ya kipuuzi na ya kitoto .
“Sasa hivi kuna watu wanasema Serikali haifanyi uamuzi mgumu sasa uwepo bila uadilifu?’ alisema.
Alisema kuwa Mwalimu Nyerere alisimamia suala la uadilifu ndiyo maana Tanzania
ilitukuka.”Ulaji rushwa ndiyo unachelewesha maendeleo, Mwalimu alisimamia sana suala hili la uadilifu ambalo ndilo linaloziharibu nchi za dunia ya tatu.
‘Uadilifu ndiyo chanzo cha mikataba ya kitoto, uamuzi mbovu…, wanaomsema Mwalimu Nyerere na kumchukia wana lao
jambo,’’ alisema Sitta.
”Uamuzi mgumu sawa, lakini hayana maana kwa nchi kama hakuna uadilifu…, suala hili siyo ‘10 percent’, hivi uamuzi mgumu maana yake ni rushwa iendelee?’ alisema.

Alichosema Nape
Naye Nape akizungumza katika mahojiano na Radio Safari Mtwara hivi karibuni alisema Serikali ya Rais Jakaya Kikwete ndiyo pekee katika nchi hii iliyokwisha kutoa uamuzi mgumu kuliko serikali zote zilizopita.
Alisema uamuzi mgumu wa kwanza uliotolewa na Serikali ya Awamu ya Nne ni kwa yeye Lowassa kulazimishwa kujiuzulu, kuvunjwa Baraza la Mawaziri, kuwafungulia kesi Kina Mramba na Yona, kuivunja Kamati Kuu ya CCM na Sekretarieti, ujenzi wa Chuo Kikuu Dodoma na ujenzi wa shule za kata.