Mchuano ya soka ya Klabu Bingwa Afrika Mashariki na Kati, maarufu kama Kombe la Kagame 2011, imeinufaisha zaidi klabu ya Yanga kwa kuvuna kitita cha takribani Sh milioni 300.
Yanga ndio waliotwaa ubingwa wa michuano hiyo iliyofanyika hapa nchini, uliokuwa ukishikiliwa na APR ya Rwanda, ikiwa ni baada ya kuichapa Simba bao 1-0 katika mchezo wa fainali uliofanyika juzi kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Kiasi hicho cha fedha, kimetokana na zawadi ya ushindi wa michuano hiyo, Dola za Marekani 30,000 (zaidi ya Sh milioni 49) na fedha walizomuuza beki wao, Nadir Haroub ‘Cannavaro’ kwa klabu ya El Merreikh ya Sudan, Dola za Marekani 150,000 (zaidi ya Sh milioni 247).
Kama ilivyokuwa kwa zawadi ya ushindi, uuzwaji wa Cannavaro umetokana na mchezaji huyo kuonekana kupitia michuano hiyo ya Kombe la Kagame.
Bila shaka, kama si michuano hiyo, Yanga isingepata kiasi hicho cha fedha, kwani hata El Merreikh wasingemwona beki wao huyo mahiri wa kati.Kwa upande mwingine, dau hilo la Cannavaro, linamfanya kuwa mchezaji ghali zaidi kuuzwa nje ya nchi, akiwapiku Mbwana Samatta na Patrick Ochan wa Simba, waliouzwa TP Mazembe ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) kwa Dola za Marekani 100,000 (zaidi ya Sh milioni 150) kila mmoja.
Kwa mujibu wa habari zilizopatikana jijini Dar es Salaam jana, El-Merreikh imemtwaa Cannavaro baada ya kocha wa timu hiyo, Hossam Elbadry, kuvutiwa na kiwango alichokionyesha katika michuano hiyo ya Kombe la Kagame.
Imeelezwa kuwa tayari viongozi wa pande hizo mbili, wameanza mazungumzo jana ili kumwezesha beki hiyo ambaye pia anachezea timu ya Taifa, Taifa Stars, kuichezea timu hiyo ya Sudan.
Chanzo cha habari kilisema kuwa Yanga imeridhia kuondoka kwa beki huyo ambapo kwa sasa El Merreikh wanachotakiwa ni kufuata taratibu za uhamisho wa mchezaji huyo, aliyejiunga na Yanga mwaka 2006 akitokea klabu ya Malindi ya Zanzibar.
Cannavaro kabla ya kutakiwa na timu hiyo, aliwahi kwenda kucheza soka ya kulipwa katika klabu ya WhiteCaps ya Vancouver ya Canada, lakini alikosa namba katika kikosi cha kwanza na hivyo kurejea nchini, huku Nizar Khalfan akiendelea kukipiga katika klabu hiyo.
Alipoulizwa jana juu ya hilo, Elbadry alikiri kuwepo kwa mazungumzo baina yao na viongozi wa Yanga ambayo yaliendelea jana jijini.
Katika michuano hiyo ya Kagame, El Merreikh walishika nafasi ya tatu baada ya kuifunga St George ya Ethiopia mabao 2-0, ikiwa ni baada ya kutolewa na Simba katika hatua ya nusu fainali kwa mikwaju ya penalti 5-4.
0 Comments