WAZIRI Mkuu Mizengo Pinda ameliambia Bunge kuwa serikali ya Awamu ya Nne haiogopi kufanya maamuzi na imeshafanya maamuzi mengi magumu.

Alikuwa akijibu hoja za wabunge waliochangia hotuba ya bajeti ya Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, akiwamo aliyekuwa Waziri Mkuu, Edward Lowassa ambaye aliituhumu Serikali kwa kushindwa kufanya maamuzi magumu.


Akizungumza kwa mara ya kwanza bungeni tangu alipojiuzulu wadhifa huo kwa kashfa ya Richmond Februari 7 mwaka 2008, Lowassa aliishangaa Serikali kwa kuogopa kufanya maamuzi.


Lowassa aliyeshika Uwaziri Mkuu Desemba 30, mwaka 2005 akiwa Waziri Mkuu wa Kumi nchini, akiichambua zaidi Serikali bungeni hivi karibuni alisema viongozi wa Serikali wameingiwa na ugonjwa wa kuogopa kutoa maamuzi kwa mambo mbalimbali hatua inayokwamisha utekelezaji wa miradi ya maendeleo.


Lakini katika majibu yake ya jana jioni, Pinda alisema Serikali haina cha kuogopa na kwamba tayari imeshafanya maamuzi mengi tena mengine ni magumu.


Alisema moja ya maamuzi hayo ni uamuzi wa kuvunja Baraza la Mawaziri uliotokana na yeye Lowassa kujiuzulu.


“Halikuwa jambo jepesi hata kidogo bali ni moja ya maamuzi mazito ambayo yamefanywa na Serikali ya Awamu ya Nne. Inataka Moyo…” alisema Pinda.


Pinda alisema maamuzi hayo ni sehemu ya maisha ya Serikali katika kutekeleza majukumu yake kwa dhana ya Uwajibikaji wa pamoja, yaani Collective Responsibility kupitia Baraza la Mawaziri.


“Tunachohitaji ni kuvumiliana. Kuvuta subira, kwani mambo mema hayataki haraka! Tutaamua na tutafanya,” alisema Pinda na kuongeza; “Napenda kulifahamisha Bunge lako Tukufu kwamba Serikali ya Awamu ya Nne chini ya Mheshimiwa Rais Dk. Jakaya Mrisho Kikwete ndiyo pekee imefanya maamuzi magumu na mazito kuliko zote zilizopita.”


Aliyataja maamuzi mengine kuwa ni pamoja kuimarisha Utawala Bora, akitolea mfano uamuzi mgumu wa kuwafikisha mahakamani waliokuwa mawaziri wa Serikali zilizopita kutokana na tuhuma mbalimbali zinazowakabili za kutumia madaraka isivyo halali.


Baadhi ya mawaziri wa Awamu ya Tatu waliofikishwa mahakamani kutokana za matumizi mabaya ya madaraka ni pamoja na Basil Mramba aliyekuwa Waziri wa Fedha na Daniel Yona (Nishati na Madini) na aliyekuwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha, Gray Mgonja.


Pinda aliendelea kusema kwamba, Serikali ya Awamu ya Nne ndiyo iliyoamua kujenga shule za sekondari za Kata ambazo zimewezesha wanafunzi wengi kupata elimu ya sekondari.


“Leo tumeshuhudia kuwa kati ya wanafunzi 20 tuliowapongeza kwa kufanya vizuri kwenye mitihani ya kidato cha sita 2011, saba (7) wanatoka shule za Kata, sawa na asilimia 35,” alisema.


Aliongeza kuwa, wameweka historia ya kuamua kujenga Chuo Kikuu cha Dodoma ambacho ni kikubwa mno nchini na kwamba faida yake inaonekana, kwani tayari zaidi ya wanafunzi 20,000 wanasoma kwa sasa.


“Ninaamini kila mmoja kati yetu humu ndani anaye mtoto, awe mjukuu, mjomba, shangazi, baba mdogo, ndugu, jamaa na hata rafiki tu ambaye anasoma katika chuo hiki.


Ndiyo sababu kubwa inayotufanya wote tuone uchungu wa baadhi ya watu wanaowasumbua hivyo kusababisha watoto wetu washindwe kukamilisha masomo yao kwa wakati kutokana na migomo inayojitokeza mara kwa mara.


“Aidha, tunajenga Chuo cha Serikali za Mitaa Hombolo ambacho kimefikia hatua nzuri,” alisema Pinda na kuongeza kuwa Serikali ya Awamu ya Nne imekamilisha miradi yote 27 ya barabara kuu zilizoanzishwa na Serikali ya Awamu ya Tatu.


Sasa hivi unaweza kutoka Mtwara-Dar es Salaam-Dodoma hadi Mwanza kwa kupitia kwenye barabara ya lami.


Alisema pia kwamba, Serikali imeamua fedha zote za MCC zipelekwe kujenga barabara za mikoa iliyoko pembezoni.


“Tumeshuhudia ndani ya Bunge hili waheshimiwa wabunge, bila ya kujali itikadi za vyama wakisifu maendeleo yaliyopatikana kule Kigoma.


Maamuzi mengine ni Ujenzi na ukamilishaji wa miradi ya maji cchini. Tumefanya maamuzi mazito katika kuwalinda watu wenye ulemavu wa ngozi na tumefanikiwa,” alisema.


Waziri Mkuu alisema ili kuondoa mpasuko wa kisiasa Zanzibar, “tumefanya maamuzi magumu ya kukubali kuanzisha Serikali ya Umoja wa Kitaifa katika Serikali ya Mapinduzi Zanzibar. Tumefanikiwa na Ulimwengu ulitusifia kwa hilo.


“Tumefanya maamuzi ya kupanua na kushamiri kwa demokrasia nchini kwa kiwango kikubwa. Nadhani, hii ndilo linasababisha baadhi yetu sasa tunajisahau na kuanza kutumia maamuzi hayo visivyo. Tunahamasisha maandamano huku tukijisifu kwamba huo ndio uzalendo. Nimeona niyataje yote haya ili kuthibitisha ukweli kwamba maamuzi yanafanyika tena kwa wakati na kwa manufaa ya wananchi wetu,” alisema Waziri Mkuu Pinda.


Pia alisema wamefanya maamuzi ya kuruhusu uhuru mkubwa wa vyombo vya habari. Mtu anaandika anachotaka, na uhuru wa kusema lolote.


“Hivi karibuni tumefanya uamuzi wa kuruhusu kuanzisha mchakato wa kupata Katiba Mpya. Hili nalo siyo jambo dogo hata kidogo,” alisema Pinda.


Awali Serikali ilisema kwa mujibu wa Katiba, Rais pekee ndiye anayeweza kubadili mfumo wa Serikali kwa sababu zozote zile atakazoona zinafaa, imeelezwa.


Imesema pia ni Rais, Jakaya Kikwete pekee ndiye mwenye mamlaka ya kikatiba ya kupunguza idadi ya wizara ili kufanya Serikali kuwa na idadi ndogo ya mawaziri na kuipunguzia matumizi ya fedha.


Hayo yalisemwa na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Uratibu na Bunge), William Lukuvi alipokuwa akitoa majumuisho ya sehemu ya hotuba ya Bajeti ya Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, kwa mwaka huu wa fedha aliyoiwasilisha Alhamisi ya wiki iliyopita.


Jibu hilo la Serikali lilitokana na hoja iliyowasilishwa na Mbunge wa Monduli na Waziri Mkuu wa zamani, Edward Lowassa (CCM) aliyeshauri baadhi ya wizara kuondolewa kwenye Ofisi ya Waziri Mkuu, ili kuipunguzia mzigo.


Akichangia kwenye hotuba hiyo ya Waziri Mkuu wiki iliyopita, Lowassa, alisema Ofisi ya Waziri Mkuu imerundikiwa wizara nyingi bila sababu hatua inayosababisha kusuasua kwa utendaji wa ofisi hiyo na kuchelewesha maendeleo.


Katika mchango wake, Lowassa alishauri Wizara ya Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi) kuondolewa kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu ili kuifanya kuwa huru na kuondoa urasimu unaotokana na mlolongo wa ngazi za uamuzi.


Lukuvi alisema,”kwa mujibu wa Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, ni Rais pekee mwenye mamlaka ya kubadili mfumo wa muundo wa Serikali kwa kuhamisha wizara kutoka sehemu moja kwenda nyingine.


Hoja hii ilitolewa na Mheshimiwa Lowassa, naomba niseme hivyo na niishie hapo,” alisema Lukuvi.