RAIS Mstaafu wa Awamu ya Pili, Alhaj Ali Hassan Mwinyi amesema kuwepo kwa viongozi wabovu duniani kumesababishwa na kutomjua Mwenyezi Mungu, na kueleza kuwa Tanzania inahitaji viongozi wacha Mungu ili kufanya uamuzi wenye kuwasaidia wananchi.

Alhaj Mwinyi aliyasema hayo jana katika mashindano ya kusoma na kuhifadhi kichwani Korani tukufu kwa vijana kutoka nchi za Afrika yaliyofanyika kwenye Ukumbi wa Diamond Jubilee, Dar es Salaam.

Katika hotuba yake kwa waumini wa dini ya Kiislamu waliokusanyika katika ukumbi huo, Alhaj Mwinyi alisema kutomjua Mungu na dini kwa ujumla, kunasababisha kupata viongozi wasiokuwa waadilifu. 

“Ukisoma Korani utamjua Mwenyezi Mungu, madhara ya kutosoma kitabu hiki kitakatifu ni kuwa na viongozi wasiokuwa waadilifu,” alisema Alhaj Mwinyi.

“Kuwa na viongozi wasiokuwa waadilifu kunasababisha kuwa na Serikali za hovyo zisizojali matakwa ya wananchi, wananchi wanapolalamika tunatakiwa tujue tatizo liko wapi, ni kurejea kwa Mwenyezi Mungu,” aliongeza Alhaj Mwinyi ambaye pia ni Mlezi wa Jumuiya ya Kuhifadhi Korani Tanzania.

Kwa mujibu wa Mzee Mwinyi, dini ni kiungo kati ya roho na matendo ya kila siku ya mwanadamu.

“Ukiijua dini vizuri utakuwa na roho iliyotakata, roho iliyotakata itasafisha matendo yako na kuwa mtu safi mwenye manufaa kwa jamii inayokuzunguka na Taifa kwa ujumla,” alisema.

Aidha, Alhaj Mwinyi aliyepachikwa jina la Mzee Ruksa wakati akiwa madarakani, alisema Watanzania wanahitaji kuwa na viongozi wacha Mungu kuanzia Mkuu wa Wilaya, Mkuu wa Mkoa, wabunge hadi mawaziri kwa sababu ucha Mungu huo utawasaidia kufanya uamuzi wenye kuwasaidia wananchi.

Aliwataka Watanzania na Waafrika kwa ujumla kurejea kwa Mwenyezi Mungu kwa kusoma vitabu vyake ili kujua mambo yaliyoamrishwa kufanywa na wanadamu na yale yaliyokatazwa ili kuwa na jamii iliyo safi mbele ya Mwenyezi Mungu.

Kwa upande wake, Makamu wa Rais, Dk. Mohamed Gharib Bilal amewaasa Watanzania wajenge utamaduni wa kusoma vitabu vya dini kwa sababu vitawasaidia kumjua Mwenyezi Mungu.

“Korani inakataza mabaya na kuamrisha mema, Korani inamwezesha mwananchi kujua majukumu yake, Korani ni kipimo cha ubinadamu wa mtu, hivyo nawaomba Watanzania kujenga utamaduni wa kusoma Korani ili kupata faida hiyo kubwa maishani,” alisema Dk. Bilal ambaye pia alikuwa mgeni rasmi katika mashindano hayo.

Mashindano ya kusoma na kuhifadhi Korani kichwani, yalianza Ijumaa iliyopita na kufikia kilele chake jana kwa kupata washindi watatu.

Mshindi wa kwanza ni Jahuddin Adam (Sudan) aliyepata zawadi ya Sh milioni tano; Kombo Bahi Makame (Unguja) alipewa Sh milioni tatu na Mohammad Sad Tawfiq kutoka Misri aliyezawadiwa Sh milioni mbili.

Mashindano hayo yalishirikisha nchi 14 kati ya 15 zilizoalikwa kutoka barani Afrika ambazo
ni Kenya, Uganda, Tanzania, Afrika Kusini, Msumbiji, Misri, Sudan, Somalia, Ethiopia, Burundi, Senegal, Nigeria, Rwanda na Iran.

Djibouti ilialikwa, lakini haikushiriki.