WAZIRI Mkuu Mizengo Pinda(pichani juu) amesema nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) zinaitazama Tanzania kwa jicho la husuda kutokana na tunu zilizopo na kutaka hatua za mtangamano ziangaliwe kwa uangalifu mkubwa.
Pinda alisema hayo jana, akifunga semina kwa wabunge kuhusu masuala mbalimbali yanayohusu fursa zilizopo katika EAC iliyofanyika katika Ukumbi wa zamani wa Bunge wa Pius Msekwa mjini hapa.
Akifafanua kuhusu hilo, Pinda alisema, “Tulikuwa na Jumuiya kama hii awali, ikafa na tukajifunza kutokana na makosa ikaanza hii nyingine, pia inaweza kufa vile vile, lakini jambo la msingi hapa ni kujua kuwa Tanzania tuna tunu nyingi, hawa wenzetu wanatuangalia kwa husuda”.
Alizitaja tunu hizo kuwa ni idadi ya watu ambayo ni soko kwa mataifa mengine, ardhi kubwa, amani na utulivu, vivutio vya utalii, pwani kubwa ya bahari, mito na maziwa, mambo yanayotupiwa macho kutokana na baadhi ya nchi nyingi za jumuiya kuyakosa.
“Wenzetu makwao hali si nzuri hata kidogo, wanaona hapa tuna kila tunu, hili lazima tuliangalie kwa jicho la kipekee. Sitta (Samuel, Waziri wa Ushirikiano wa Afrika Mashariki) na timu yako muhakikishe mnatetea maslahi ya nchi,” alisema Pinda.
Kuhusu elimu kwa umma, Pinda alishauri iendelee, lakini akasisitiza elimu zaidi inahitajika kwa Viongozi wa Serikali Kuu, Serikali za Mitaa, Mashirika yasiyo ya kiserikali (NGO’s), wabunge na wajumbe wa Baraza la Wawakilishi.
Wabunge wengine pia waliomba Wawakilishi Zanzibar wapatiwe semina kama hiyo wakati wakichangia hoja jana.
Awali, kabla Pinda hajafunga semina hiyo, Mwenyekiti wa semina hiyo, Mbunge wa Ilala, Mussa Azzan Zungu (CCM), alisema tayari Waziri Sitta amemhakikishia kuwa utaratibu
umeandaliwa kuwapatia semina wajumbe wa Baraza la Wawakilishi.
|
0 Comments