Bunge jana lililazimika kuahirisha shughuli zake hadi leo, kufuatia kifo cha Mbunge wa Baraza la Wawakilishi (CCM), Mussa Khamis Silima(Pichani juu), aliyefariki dunia katika Taasisi ya Mifupa ya Hospitali ya Taifa Muhimbili (MOI).
Silima alifariki dunia siku moja baada kufiwa na mkewe, Mwanakheri Ali, katika ajali ya gari iliyotokea eneo la Nzuguni, mkoani hapa Jumapili saa 2:15 usiku.
Katika ajali hiyo, Silima na dereva wake, Chezani Sembonga, walijeruhiwa na kukimbizwa katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Dodoma kabla ya kuhamishiwa MOI juzi.
Taarifa za kufariki kwa mbunge huyo ambaye pia alikuwa Mwakilishi wa Jimbo la Uzini, zilitangazwa jana saa 5:50 asubuhi na Spika wa Bunge, Anne Makinda, wakati wabunge walipokuwa wakiendelea kuchangia hotuba ya bajeti ya Wizara ya Maji iliyowasilishwa juzi na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, (Mahusiano na Uratibu), Steven Wasira.
Spika akinukuu kanuni ya 33 (2) ambayo kinasema: “Wakati wa kikao, Spika anaweza kutoa taarifa bungeni nyinginezo kadri atatakavyoona inafaa,” alisema na kuongeza:
“Jana (juzi) niliwapa taarifa kuhusu ajali ya Mbunge mwenzetu eneo la Nzuguni na kwamba mke wake alifariki papo hapo. Na kwamba dereva wake na Silima walipata majeraha makubwa na wamepelekwa Muhimbili kwa matibabu zaidi. “Leo asubuhi kabla ya kuanza maswali nilitoa taarifa kwenu wabunge kuwa nimeongea naye akiwa anaendelea kupata matibabu, ni kweli nimeongea naye na kwa masikitiko makubwa naomba kuwatangazieni kuwa:
“Nimepokea taarifa kutoka kwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii, kuwa Mheshimiwa Mussa Khamis Silima amefariki dunia muda mfupi uliopita.”
“Kwa mujibu wa kanuni ya 149 ya Bunge toleo la 2007, naahirisha shughuli za Bunge mpaka kesho (leo) saa tatu asubuhi,” alisema Spika kwa uchungu na kisha kuagiza kukutana na wajumbe wa Kamati ya Bunge ya Uongozi kuzungumzia na kupanga shughuli za msiba huo.
Nje ya Bunge wabunge kadhaa walionekana kukaa vikundi vikundi wakizungumzia msiba huo.
Spika akielekea kwenye kikao cha uongozi, alizungumza na baadhi ya wabunge na waandishi wa habari na kueleza kuwa anahisi taarifa za kifo cha mkewe Mwanaheri Ali, zimechangia kifo cha Mbunge huyo.
Juzi Silima akizungumza na baadhi ya wabunge na waandishi wa habari katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Dodoma, alisema wakati ajali hiyo ilipotokea mkewe (ambaye ni marehemu), alipoteza fahamu na kwamba akipata nafuu atakwenda kumjulia hali.
Jana asubuhi kabla ya kuanza kipindi cha maswali na majibu, alilitangazia Bunge kuwa amezungumza naye na kumpa taarifa kuhusu kifo cha mkewe na alizipokea vizuri.
Taarifa zilizopatikana kutoka Muhimbili zilieleza kuwa, alipotaarifiwa kuhusu kifo cha mkewe, hali ilibadilika ghafla na muda mfupi baadaye alifariki dunia. Silima na mkewe Mwanaheri pamoja na mtumishi wa ndani Mwanahamisi, walipata ajali mbaya katika eneo la Nzuguni, Dodoma juzi usiku wakitokea Dar es Salaam baada ya kuhudhuria mazishi ya shemeji yake na kusababisha kifo cha mkewe.
Mwanahamisi alipata michubuko midogo na alipata matibabu hospitali ya Dodoma kisha akauruhusiwa.
Wakitoa maoni yao kwenye viwanja vya Bunge, baadhi ya wabunge walisema wamesikitishwa sana na kifo hicho. Mbunge wa Makete (CCM), Dk. Binilith Mahenge, alisema anaamini kuwa ndiyo mapenzi ya Mungu na kwamba ni vigumu kutoa maoni kwa kuwa hawana taarifa za kina jinsi ajali hiyo ilivyotokea.
“Hatuwezi kutoa coment (maoni) yoyote maana hatufahamu jinsi ajali hiyo ilivyotokea, lakini ndiyo Mwenyezi Mungu ndiye mwenye uwezo ameondokewa na mkewe na sasa yeye mwenyewe,” alisema.
Mbunge wa Kisarawe (CCM), Selemani Jafo, alisema kuwa taarifa za kifo hicho kimewashtua sana wabunge.
“Tumepoteza familia nzima, ameacha watoto ambao pengine kuna wengine wanasoma huwezi kujua familia iliyobakia inapokeaje hali hiyo. Changamoto ni serikali ama Bunge limejipanga vipi kuwahudumia watoto hawa ambao baba yao alikutwa na mauti wakati anawatumikia wananchi,” alisema.
Waziri Mkuu, Mizengo, Pinda, alisema kifo hicho ni tukio la kusikitisha, lakini ni jambo lisiloweza kuzuilika kwani ni mapenzi ya Mungu.
UTARATIBU WA MAZISHI WATANGAZWA
Kaimu Katibu wa Bunge, John Joel, alisema mwili wa marehemu ulisafirishwa kwa ndege kuelekea nyumbani kwake Zanzibar jana kati ya saa 10:00 na saa 11:00 jioni.
Alisema kuwa mazishi ya mbunge huyo yatafanyika leo saa 7.00 mchana kisiwani Zanzibar.
Taarifa kutoka Zanzibar zinasema kuwa mwili wa Silima uliwasili visiwani hapa na kupelekwa moja kwa moja Baraza la Wawakilishi, Chukwani ambako wawakilishi walimuaga. Akizungumza na NIPASHE jana jioni, Mbunge wa Uzini jimbo alilotoka marehemu, Mohammed Seif Khatib, alisema baada ya kuagwa barazani mwili huo ulipelekwa kijijini kwa marehemu Kiboje ambako utalazwa na mazishi yatafanyika leo saa saba mchana.
Awali Kaimu Katibu wa Bunge Joel alisema wawakilishi wa Bunge 57 kutoka Kamati ya Uongozi, Tume ya Bunge, Kamati ya Nishati ya Madini ambayo marehemu alikuwa mjumbe na wabunge wanaotokea Zanzibar na wale wa Bara watakwenda kuhudhuria mazishi.
Pia alisema msafara huo ambao utaongozwa na Spika Makinda utawashirikisha waandishi wa habari watatu.
Alisema wawakilishi hao wataondoka katika uwanja wa ndege wa Dodoma leo saa 4:00 asubuhi na kurejea tena mjini hapa mara baada ya kukamilika kwa shughuli za mazishi.
DEREVA WAKE AENDELEA VIZURI
Wakati huo huo, dereva wa marehemu Sembonga, anaendelea kupatiwa matibabu MOI ambapo imeelezwa hali yake inazidi kuimarika.
Ofisa Uhusiano wa MOI, Almas Jumaa, alisema Sembonga anaendelea na matibabu na juhudi za kumfanyia upasuaji zinafanyika. “Tunaendelea na jitihada za kuunga mguu wake uliovunjika, lakini kwa ujumla hali yake inaendelea vizuri,” alisema Jumaa.
JK ATUMA SALAMU
Rais Jakaya Kikwete ametuma salamu za rambirambi kwa Spika wa Bunge, Anne Makinda, na Spika wa Baraza la Wawakilishi Zanzibar, Pandu Ameir Kificho, kutokana na kifo cha Silima.
“Nashindwa kupata maneno fasaha ya kuelezea ipasavyo huzuni yangu na mshituko wangu kufuatia habari za kifo cha Mheshimiwa Silima. Hili ni pigo kubwa lisiloweza kuzibika kwa urahisi katika Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Baraza la Wawakilishi Zanzibar, na kwa kweli Tanzania Bara na Tanzania Zanzibar kwa ujumla,” alisema Rais Kikwete katika salamu zake na kuongeza:
“Nilimfahamu Marehemu Silima enzi za uhai wake kutokana na utumishi wake uliojaa uadilifu katika nyadhifa mbalimbali alizowahi kuzitumikia katika Jumuiya ya Wazazi hadi kufikia wadhifa wa Naibu Katibu Mkuu, Mwakilishi wa Jimbo la Uchaguzi la Uzini na hatimaye Mbunge wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia Baraza la Wawakilishi.”
CHANZO: NIPASHE

0 Comments