Gari hii ndiye aliyekuwamo marehemu  Silima na marehemu Mkewe Silima.

Mahakama ya Wilaya ya Ilala jana ililazimika kuhamishia ofisi yake katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili kumsomea mashtaka dereva Cherzad Sebunga (30), ya kusababisha kifo cha aliyekuwa Mwakilishi Mussa Khamis Silima (CCM) na mke wake.
Mshtakiwa huyo alisomewa mshataka yake katika wodi binafsi namba 2, ambapo ilidaiwa na Mwendesha Mashtaka Wakili wa Serikali, Nassoro Katuga, mbele ya Hakimu Mkazi Mfawidhi, Joyce Minde, kuwa Agosti 21, mwaka huu, katika barabara ya Morogoro na Dodoma eneo la Nane Nane Nzunguni, mshtakiwa alitenda kosa.
Ilidaiwa kuwa siku hiyo mshtakiwa akiwa dereva na kiongozi wa gari namba T509 AJC aina ya Toyota Corolla, aliliendesha kwenye barabara ya umma kwa namna ambayo kwa mujibu wa mazingira ya kesi hii, ilikuwa ni hatari kwa umma na watumiaji wengine wa barabara.
Ilidaiwa kuwa kutokana na uendeshaji huo, alishindwa kuchukua tahadhari inayotakiwa wakati akilipita gari namba T330 AYF aina ya Isuzu ERF likiwa na tela namba T 673 ATS na kuligonga.

Pia ilidaiwa kuwa, mshtakiwa aligongana na gari jingine lenye namba T497 ASW aina ya Scania lililokuwa likitokea mbele yake na kusababisha kifo cha Mwakilishi huyo na mkewe, Mwanaheri Twalibu waliokuwa ni abiria katika gari hilo.
Mshtakiwa alikana kutenda kosa hilo na kurudishwa rumande baada ya kushindwa kutimiza masharti ya dhamana.
Masharti ya dhamana yalimtaka kuwa na wadhamini watatu wanaoishi Dar es Salaam, ambao watasaini bondi ya Shilingi milioni tatu.
Kesi hiyo iliahirishwa hadi Septembe 8, mwaka huu itakapotajwa tena.
CHANZO: NIPASHE