Msanii wa kizazi kipya, Diamond Platinumz, aliwateka mashabiki wake wa Shule ya Sekondari ya Sangara katika shoo maarufu ya kuvumbua vipaji inayoandaliwa na kituo cha televisheni cha East Africa Television (EATV) iitwayo ‘5 Selekt’ iliyofanyika mwishoni mwa wiki.
Shoo hiyo iliyotawaliwa na kelele za furaha zilifika kileleni pale msanii huyo mkali ajulikanaye kama ‘Raisi wa Wasafi’ alipopanda jukwaani akiwa ameambatana na wacheza shoo wake wanne.
Msanii huyo aliimba nyimbo zake mbalimbali zinazotamba zikiwemo Nenda kwa Mwambie, Nitarejea na Mbagala uliompa umaarufu hapa nchini.

 
Diamond ambaye pia huwa sambamba na wacheza shoo wake katika kuonyesha umahiri wake aliweza pia kuwafurahisha wanafunzi waliokuwa wanamshangilia na vile vile kuwataka wanafunzi hao kuweka mkono mmoja juu kama ishara ya umoja.
Aidha waandaji wa shoo hiyo EATV waliweza kuwa tunuku wanafunzi zawadi zikiwemo fulana, madaftari na kalamu zote zenye nembo ya kituo chao cha EATV.
Vilevile wadhamini wa shoo hiyo kampuni ya huduma za simu ya Airtel pia iliwazawadia wanafunzi wa shule hiyo fulana, madaftari na kofia.
Shoo hiyo hufanyika kila Ijumaa ya kwanza mwezi ambapo lengo lake ni kuibua vipaji mbalimbali vya sanaa kama kuimba, kuonyesha mavazi na kucheza muziki.