Waziri Kivuli wa Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Halima Mdee mwenye kipaza sauti.

Marais wawili na mawaziri wakuu wawili wastaafu wamelipuliwa bungeni kwamba wamemilikishwa maeneo makubwa ya ardhi ya wananchi katika Halmashauri ya Wilaya ya Mvomero mkoani Morogoro na kuyaacha bila kuyaendeleza.
Waliotajwa ni Rais Mstaafu wa awamu ya pili, Ali Hassan Mwinyi; Rais wa awamu ya tatu, Benjamin Mkapa; Waziri Mkuu na Makamu wa Kwanza wa Rais Mstaafu wa awamu ya pili, John Malecela na Waziri Mkuu Mstaafu wa awamu ya tatu, Frederick Sumaye.
Wengine waliotajwa kumilikishwa maeneo makubwa ni Katibu Mkuu Mstaafu wa Chama Cha Mapinduzi, Philip Mangula na Waziri wa zamani wa Nchi, Ofisi ya Rais (Tamisemi), katika serikali ya awamu ya tatu, Brigedia Jenerali Mstaafu Hassan Ngwilizi.
Hayo yalisemwa bungeni jana na Msemaji Mkuu wa Kambi ya Upinzani ambaye pia ni Waziri Kivuli wa Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Halima Mdee, wakati akitoa maoni ya kambi hiyo katika hotuba ya makadirio ya matumizi ya Wizara hiyo kwa mwaka wa fedha wa 2011/12 iliyosomwa na waziri wake, Profesa Anna Tibaijuka.
Mdee alisema kuwa matatizo ya ardhi kwa wakubwa kunyang’anya wanyonge ardhi imeikumba Halmashauri ya Wilaya ya Mvomero na kwamba mgogoro huo unahusu shamba namba 299 (iliyokuwa ranchi ya NARCO), lenye ukubwa wa hekta 49,981.
Alisema kuwa katika shamba hilo, taarifa zinaonyesha kwamba hekta 30,007 walipewa Mtibwa Sugar licha ya malalamiko kutoka kwa wananchi kwamba eneo walilopewa ni kubwa sana.
Mdee ambaye ni Mbunge wa Kawe (Chadema), alisema kuwa taarifa za kiuchunguzi zinaonyesha kwamba maeneo ambayo yalikuwa yamepangwa kugawiwa wanakijiji wa kijiji cha Wami, yamegawiwa kwa vigogo hao.

Alisema kuwa Mangula anaongoza kwa kuwa ‘mwanakijiji’ mwenye eneo kubwa, alipewa hekta 2,000, Malecela hekta 100 na Ngwilizi hekta 100 kati ya hekta 5,000, zilizosemwa wamepewe wakulima wadogowadogo wa kijiji.
Alisema kuwa Mwinyi anamiliki hekta 2,000, ambazo hazijaendelezwa, Sumaye hekta 500 na Mkapa hekta 1,000.
Hata hivyo, Mdee aliliambia Bunge kuwa ni Mkapa pekee ambaye shamba lake limeendelezwa tofauti na wengine ambao hawajayaendeleza mashamba waliyopewa.
“Mheshimiwa Spika, Kambi ya Upinzani inahoji, kama hawa watajwa hapo juu ni wakazi wa kijiji cha Wami- Dakawa? Na ni vigezo gani vilitumika kuwanyima ardhi wanakijiji na kuwapa wakubwa hawa? Serikali haioni kwamba mgao huu wa ardhi uliojaa dhuluma na upendeleo unahatarisha maisha ya Watanzania na usalama wa nchi kwa ujumla?”
“Mheshimiwa Spika, wananchi wa maeneo haya wana hasira na serikali yao kwa kuwa wameshaambiwa hakuna tena eneo la kugawa, wakati walitozwa Sh. 20,000 kila mmoja kwa madai kwamba wangepewa hekta 5. Ahadi ya hekta 10,019 kwa wakulima na wafugaji, imegeuka hewa! Tunakwenda wapi kama nchi?” alihoji Mdee na kuongeza:
“Mheshimiwa Spika, Kambi ya Upinzani inaitaka serikali kuangalia upya zoezi la ugawaji wa ardhi katika maeneo yote yenye utata! Ambayo yalitawaliwa na rushwa, ubabe na udanganyifu.”
Kuhusu migogoro ya ardhi nchini, alisema hivi sasa imekithiri kufikia hatua ya uvunjifu wa amani na kufikia hadi umwagaji damu na pengine vifo kutokea katika maeneo kadhaa.
Alisema: “Hali hii imeondoa utamaduni wetu wa asili wa kuvumiliana na kumaliza matatizo yetu kwa njia mwafaka na mazungumzo. Ni muhimu serikali ikaelewa kwamba kupuuza migogoro hii ya ardhi nchini ni sawa na kuatamia bomu, hivyo ni lazima hatua za haraka zichukuliwe.”
Mdee alisema migogoro hasa ya wananchi na wawekezaji inakua kwa kasi na kuchukua sura mpya.
“Anapokuja ‘mgeni’, kwa jina la ‘Mwekezaji’ matendo ya Serikali yetu yanapingana na usemi usemao ‘mgeni njoo mwenyeji apone’, bali imekuwa ‘mgeni njoo mwenyeji asulubike’,” alisema.
RUTABANZIBWA ASHAMBULIWA
Wabunge wawili wamemshambulia Katibu Mkuu wa Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Patrick Rutabanzibwa, kwa tuhuma mbalimbali ikiwemo kugawa hekta 25,000 za wilaya ya Mkinga mkoani Tanga kwa mwekezaji.
Wakati Rutabanzibwa akituhumiwa kugawa eneo hilo, Katibu Mkuu, Wizara ya Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), anadaiwa kuandika barua akipinga eneo hilo kugawiwa kwa mwekezaji.
Madai hayo yaliibuliwa na Mbunge wa Mkinga (CCM), Dustan Kitandula, wakati akichangia hotuba ya Waziri Tibaijuka.
Alisema hekta 25,000 za ardhi katika wilaya hiyo, zimesha gawiwa kwa wawekezaji 11 wakati wilaya hiyo inakabiliwa na ukosefu wa maeneo kwa ajili ya kilimo na ufugaji.
“Hawa watu ni watendaji wakuu wa serikali, wako katika serikali moja ya Chama Cha Mapinduzi, lakini wanatoa maamuzi yanayogongana na ushauri uliotolewa na Katibu Mkuu Tamisemi ulikuwa ni mzuri sana.”
Hata hivyo, alisema uwekezaji ni jambo zuri, lakini wananchi wa Mkinga wanaunga mkono uwekezaji ambao unafuata taratibu zinazotakiwa.
Alisema wilaya hiyo imekuwa ikikabiliwa na tatizo la wahamiaji haramu kutoka nchi za Somalia na Kenya ambao wamekuwa wakiingia kila siku na kwamba kama vile haitoshi eneo hilo linagawiwa kwa wawekezaji.
Alisema katika wilaya ya Mkinga kuna mwekezaji ambaye ni Kampuni ya Arkadia Ltd, ambayo imepewa kibali cha kumiliki hekta 25,000 kwa ajili ya kulima zao la jatropha na kibali hiki kilitolewa na Rutabanzibwa.
Hivi kweli ndugu zangu tunaitakia mema nchii hii, baadhi ya vijiji vinavyotajwa katika uwekezaji huu viko mpakani mwa nchi yetu na Kenya, tunabinafsisha ardhi ya aina hiyo wakati tukijua kuna wimbi la wageni wanaoingia nchini kiholela, hivi kweli ‘are we serious (tuko makini)?”alihoji.
“Hili hatulitaki kabisa na kwambia Mheshimiwa Waziri katika wizara yako kuna watu wanampotosha Rais, wanataka kumfanya rais aonekane mbaya kwa wananchi wa Mkinga. Kwa hiyo, nakuomba ushughulikie hili haraka,” alisema Kitandula na kukataa kuunga mkono hoja.
Mbunge wa Temeke, Abbas Mtemvu (CCM), alimshutumu Rutabanzibwa na kusema kama ataendelea kuwepo katika wizara hiyo, uwezekano wa wizara kufanikiwa ni mdogo.
Alisema Rutabanzibwa ni kikwazo katika wizara hiyo kwa kuwa ndiye anayekwamisha fidia kwa wakazi wa Kurasini Dar es Salaam waliohama makazi yao kupisha upanuzi wa Bandari ya Dar es Salam ingawa Waziri Mkuu, Mizengo Pinda na Rais Jakaya Kikwete, wamewahi kutoa maagizo kwa nyakati tofauti ili wananchi hao walipwe fidia.
“Kilio cha wananchi wa Kurasini ni Katibu Mkuu (Rutabanzibwa) hata lile eneo la mradi hajafika, ni tatizo kweli kweki si vyema kusema watu, lakini niseme kweli Katibu Mkuu huyu bwana mkubwa huyu kama ataendelea na Mama Tibaijuka kazi yote nzuri inayofanywa itakuwa ni bure,” alisema na kukataa kuunga mkono bajeti hiyo hadi aambiwe lini wakazi hao watalipwa fidia.
CHEYO ALIA NA WAWEKEZAJI
Mbunge wa Bariadi Mashariki, (UDP) John Cheyo, alisema watu wanaotoka Kanda ya Ziwa ardhi ni msingi wa kuondokana na umaskini, lakini wanaikosa.
“Sasa hivi kule Sukuma Land tumebanana, hivi tunatafuta twende tukalime wapi na serikali imezungumza Kilimo Kwanza. Ukienda kugusa hapa mwekezaji, ukienda kugusa hapa mwekezaji, ukigusa hapa uhifadhi, ukienda ukagusa hapa uhifadhi ni wapi Tanzania hii ndio tumepewa na Mungu,” alisema.
Alisema wakati umefika kwa Tanzania kupima ardhi kwa kuangalia kama mali na kutenganisha maeneo ya wawekezaji na yale yatakayokuwa kwa ajili ya wazawa.
Alitaka wawekezaji wanaokuja nchini kwa ajili ya uwekezaji kutopewa ardhi bure kwa kuwa jambo hilo husababisha rushwa na ufisadi.
CHANZO: NIPASHE