Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu-Sera, Uratibu na Bunge, William Lukuvi

Watanzania milioni mbili wameshaambukizwa virusi vya ugonjwa wa Ukimwi, huku kiwango cha watoto yatima chini ya miaka 18 kikizidi kuongezeka mwaka hadi mwaka.
Hayo yalisemwa jana na Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu-Sera, Uratibu na Bunge, William Lukuvi wakati akifungua semina ya siku moja ya Ukimwi kwa Wabunge iliyofanyika katika ukumbi wa Pius Msekwa.
Semina hiyo iliendeshwa na Tume ya Kuthibiti Ukimwi Tanzania (Tacaids), huku Dk. Fatuma Mrisho akiwa mwezeshaji katika semina hiyo iliyohudhuriwa na wabunge wa majimbo na wale wa Viti Maalum.

Alisema kuwa ili kupunguza tatizo la Ukimwi na kuwafanya wananchi kupata uelewa zaidi kuhusu ugonjwa huo, viongozi wa Serikali na wale wa kisiasa kuongelea masuala ya Ukimwi na kuyaweka katika mipango yao ya utekelezaji.
Lukuvi alisema kuwa kutokana na juhudi mbalimbali za Serikali matokeo ya mafanikio yameanza kujitokeza, ambapo kiwango cha maambukizi kimeshuka kutoka asilimia saba hadi 5.7 kwa mwaka 2007/2008 na jamii imekuwa na uelewa na kusababisha unyanyapaa kupungua na watu wanaweza kuongea masuala ya ukimwi bila woga.
Alisema pamoja na juhudi za Seikali kwa kupitia Tacaids, bado Serikali na Wabunge, wana jukumu kubwa la kuhakikisha Watanzania hawaendelei kuambukizwa Ukimwi.
Lukuvi aliwataka Wabunge kupeleka mapambano ya Ukimwi katika majimbo yao, kuendeleza utetezi, kuongea katika majukwaa ya kisiasa, kujitolea muda wao ili kusaidia mipango ya Ukimwi na kutumia mashirika ya kidini na asasi za kiraia zilizoko majimbo mwao kuutokomeza ugonjwa huo.
Naye mwezeshaji Dk. Mrisho alisema jumla ya Shilingi tririoni moja hutumika kila mwaka kwa shughuli za Ukimwi, ambapo fedha nyingi huenda katika ununuzi wa dawa za kurefusha maisha.
Wabunge waliuliza maswali 17 kuhusu ugonjwa wa Ukimwi na kupatiwa majibu kutoka kwa wataalam waliongozana na Tacaids.
CHANZO: NIPASHE JUMAPILI