Kamati Kuu (CC) ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), imewafukuza uanachama madiwani watano wa Jiji la Arusha kwa kukaidi agizo la chama hicho lililowataka kujiuzulu nafasi zao za uongozi na kuomba radhi kutokana na makosa waliyoyafanya kwa kuingia katika mwafaka wa umeya jijini humo.
Akizungumza mjini hapa, Mwenyekiti wa chama hicho, Freeman Mbowe, alisema uamuzi huo umefikiwa na Kamati Kuu iliyofanya kikao cha dharura juzi na jana mjini hapa.
Madiwani waliofukuzwa uanachama ni Estomih Malaah (kata ya Kimandolu) ambaye alikuwa Naibu Meya wa Jiji hilo katika mwafaka huo na mwenyekiti wa madiwani wa Chadema jijini Arusha.
Wengine ni John Bayo (Elerai) ambaye alikuwa mnadhimu wa madiwani wa Chadema na katika mwafaka huo alipewa cheo cha Mwenyekiti wa Kamati ya Elimu, Afya na Uchumi.
Charles Mtanda (Kaloleni), Reuben Ngowi (Themi) ambaye alikuwa mjumbe wa kamati ya fedha katika halmashauri hiyo na Rehema Mohamed (Viti Maalum).
Alisema madiwani waliotimuliwa ni madiwani watano kati ya 10 ambao walitekeleza maelezo ya CC iliyokutana Julai 17 mwaka huu.
Mbowe alisema Kamati Kuu imezingatia kuwa kitendo cha kukataa kutekeleza maagizo halali ya Kamati Kuu ni utovu mkubwa wa nidhamu na ni kuvunja maadili na kanuni za chama na kinaenda kinyume cha msingi wa Chadema wa uwajibikaji.
“Hatufurahii kuwafukuza madiwani wetu ni uamuzi ambao tuliufanya kwa kujali maslahi na mustakabali wa taifa hili, uongozi ni dhamana na sisi viongozi wa Kamati Kuu kwa wajibu tuliopewa na katiba ya chama wajibu wetu wa msingi ni kusimamia utekelezaji wa katiba, kanuni na maadili ya chama,” alisema na kuongeza:
“Kwa uchungu mkubwa sana baada ya juhudi zote kushindikana tumelazimika kuwafukuza madiwani wetu watano ili kuweka nidhamu ndani ya chama ili kuthibitisha kwa vitendo ndani ya Chadema hakuna aliye juu ya chama chetu, Mwenyekiti nikifanya makosa ya utovu wa nidhamu ninawajibishwa kwa mujibu wa katiba ya chama hiki.”
Alisema atakapotokea mtu yeyote ambaye atakiuka waziwazi na kukaidi maagizo ya vikao halali vya chama hawatasita kumchukulia hatua hata kama akiwa mwenyekiti, makamu, katibu mkuu, mbunge ama diwani.
“Ila hatutachukua maamuzi yoyote bila kufuata katiba, hatutachukua maamuzi yoyote bila kumpa mtu fursa zote kisheria na hata kijamii za kumshawishi na kumshauri, madiwani wetu tulichukua hatua hii baada ya juhudi zote tulizozifanya kama Kamati Kuu kushindikana,” alisema.
Mbowe alisema kuwa: “Uamuzi tuliouchukuwa wa kuwaondoa udiwani wanachama watano ni uamuzi mzito sana na hauna siri wala kificho na sisi kama chama hatuogopi kufanya maamuzi.”
Alisema madiwani hao walijulishwa maamuzi ya Kamati Kuu ndani ya kikao hicho cha CC Agosti 7 mwaka huu (jana) saa 7:45 usiku na kwamba kila mmoja atakabidhiwa barua yenye kueleza maamuzi ya Kamati Kuu.

KAMATI KUFUNIKA ARUSHA
Alisema chama kimewaagiza viongozi waandamizi waende Arusha kuzungumza na wananchi wote ambao wameathiriwa na kufukuzwa kwa madiwani hao.
Alisema chama hicho kimeandaa mkutano mkubwa wa hadhara mjini Arusha Alhamisi wiki hii na kwamba mkutano huo utaongozwa na yeye (Mbowe), Kwa kushirikiana na Katibu Mkuu wa chama hicho, Dk. Willibroad Slaa, Naibu Katibu Mkuu, Zitto Kabwe na wajumbe wa CC.
Aliwataja wajumbe hao wa CC watakaokwenda kuhutubia mkutano huo kuwa ni Mbunge wa Iringa Mjini, Mchungaji Peter Msigwa; Mbunge wa Viti Maalum, Regia Mtema; Mwenyekiti wa baraza la Vijana Taifa wa chama hicho, Heche Suguta; Mbunge wa Viti Maalum, Chiku Abwao na Mbunge wa Nyamagana Ezekia Wenje.
Wengine ni Mbunge wa Singida Mashariki na Mnadhimu wa kambi ya upinzani bungeni, Tundu Lissu; Meya wa Manispaa ya Musoma, Kasululu Malima; Mwenyekiti wa Halmashauri ya Karatu, Lazaro Masai, na Mwenyekiti Manispaa ya Moshi, Jaffar Maiko.
Pia watakuwapo Mbunge wa Arusha Mjini, Godbless Lema na madiwani wengine wa Jiji la Arusha.
Akizungumzia hatma ya Diwani wa Sekei, Cyprian Tarimo, ambaye juzi hakuweza kufika kuhojiwa na CC, Mbowe alikiri kupokea taarifa ya udhuru wake na ilipokelewa na Kamati Kuu.
“Lakini kwa sababu Chadema ni chama cha kutenda haki hatuwezi kumhukumu mtu bila kumsikiliza, kuhukumu ama chochote kitakachoamuliwa kuhusiana na diwani huyu kitafanyika baada ya kuwa tumemsikiliza,” alisema Mbowe.
Kuhusu kama wanaweza kuomba tena uanachama, alisema bado wanachama hao wanauwezo wa kukata rufaa baraza kuu na hatimaye mkutano mkuu.
“Lakini tumewaadhibu kwa kupingana na mambo ya msingi ya maamuzi ya vikao halali vya chama wakakataa kuomba radhi, wakakataa maelekezo sasa chama cha siasa ambacho hakiwezi kuelekeza madiwani ni chama cha kihuni sio chama cha siasa, katika mazingira kama hayo tulikuwa hatuna chaguo, lazima kuchukua hatua,”alisema.
Alipohojiwa kwa njia ya simu Malaah, alisema kuwa anakusudia kukata rufaa katika vikao vya juu vya chama hicho mara baada ya kupata barua rasmi ya chama.
Alisema kuwa atakata rufaa kwa kuwa hawakutendewa haki na kikao hicho cha CC na kuongeza kwamba hata taarifa ya tume iliyokwenda kuwachunguza ambayo walistahili kupewa, hawakupewa.
“Tume ilikuja kutuchunguza kule Arusha lakini hadi leo sisi madiwani hatujapewa ripoti yake.”
Kwa upande wake, Bayo alisema mgogoro wa Arusha hauwahusu wao wala CC, bali ulikuwa ukiwahusisha wao na Mbunge wa Arusha Mjini, Lema.
“Ugomvi wetu si baina ya CC na sisi bali tumetofautiana na Lema katika mambo mengi …mimi sina ugomvi na viongozi wangu nawaheshimu, pamoja na kuvuliwa uanachama nitaendelea kuwa Chadema damu damu,”alisema.

MAZUNGUMZO NA WAZIRI MKUU
Katika hatua nyingine, Mbowe alisema kuwa CC imepokea taarifa ya mazungumzo ya kamati ya Waziri Mkuu, Mizengo Pinda na yeye pamoja na Katibu Mkuu wa Chama hicho, Dk. Slaa, kuhusu tatizo la mgogoro wa umeya Jiji Arusha.
Alisema mazungumzo hayo yaliofanyika nyumbani kwa Waziri Mkuu juzi mjini Dodoma, Pinda alikubali kuundwa kwa kamati ya kitaifa ya kushughulikia mgogoro huo.
Alisema kamati hiyo itajumuisha pande mbili zinazohusika katika mgogoro huo ambazo ni CCM na Chadema.
“Kamati ya Kitaifa ya maridhiano itaundwa haraka iwezekanavyo na kwa vyovyote mgogoro wa umeya wa Jiji la Arusha tulikubaliana uishe ndani ya mwezi mmoja tangu tarehe ya mazungumzo ya Mwenyekiti wa Taifa na Waziri Mkuu,”alisema.
Alisema Mwenyekiti wa kamati hiyo ya kitaifa atakuwa Msajili wa Vyama vya Siasa, John Tendwa na kwamba yeye ndiye atakayeratibu uundwaji wa kamati hiyo.
Alisema kuwa mara baada ya kumalizika kwa mgogoro wa umeya Arusha, CC imewaagiza waanze kuhudhuria vikao vya Halmashauri ya Jiji la Arusha.
Madiwani hao waliingia mwafaka na wenzao wa CCM kwa makubaliano ya kugawana madaraka kwenye halmashauri. Chadema walipewa nafasi ya Naibu Meya, ambayo wangeshikilia kwa miaka minne kisha kumwachia diwani wa TLP; pia waligawana kamati za baraza la madiwani.
Hata hivyo, Mbunge wa Arusha Mjini, Lema, aliukana mwafaka huo na baadae Kamati Kuu ya Chadema iliagiza madiwani walioingia katika mwafaka huo wajiuzulu nafasi walizochukua na kuomba radhi.
Madiwani hao waligoma kuomba radhi kama walivyoagizwa na CC ya chama hicho.

CHIMBUKO LA MGOGORO
Mgogoro wa umeya uliibuka mwaka jana baada ya Chadema kupinga uchaguzi wa meya wa Jiji hilo ambao walisema ulikiuka taratibu na sheria za uchaguzi.
Katika kupinga uchaguzi huo, Chadema walifanya maandamano makubwa mjini Arusha Januari 5, mwaka huu ambayo yalizimwa na polisi na kuishia kuuawa kwa watu watatu waliopigwa risasi na polisi katika maeneo mbalimbali ya jiji hilo.
Aidha, viongozi waandamizi wa Chadema akiwamo Mwenyekiti Mbowe; Katibu Mkuu Dk. Slaa, wabunge, Lema; Philemon Ndesamburo (Moshi Mijini) na wengine walikamatwa na kufunguliwa mashtaka mahakamani. Kesi hiyo bado inaendelea.
CHANZO: NIPASHE