Hofu kubwa iliwakumba abiria zaidi ya 400 baada ya moto kulipuka katika meli ya MV. Sea Gull ilipokuwa ikisafiri kutoka Zanzibar kwenda Dar es Salaam usiku wa kuamkia juzi.
Abiria waliokuwemo ndani ya meli hiyo walisema moto huo ulioanza kubainika katika eneo la kuhifazia mizigo hali iliyosababisha mtafaruki mkubwa miongoni mwa abiria.
“Hivi ninavyoongea na wewe mabaharia wanajaribu kuuzima kwa kutumia vifaa vya kuzimia moto na mizigo mingine inatupwa baharini,” alisema abiria mmoja Ali Hamad.
Hata hivyo, alisema kutokana na mabaharia wa meli hiyo kukosa sare abiria hao waliokuwemo melini walikuwa na wakati mgumu na kushindwa kuwapata wafanyakazi wa meli ambao wangeweza kuwapa msaada.
Aidha, alisema pamoja na meli hiyo kuwa na huduma za televisheni, lakini mikanda ya sinema ndio imekuwa ikiwekwa badala ya ile inayotoa elimu kwa abiria juu ya kujilinda inapotokea hali ya dharura.
“Hali si nzuri kwa sababu abiria ni wengi kupita kiwango, wengine wanalia kama unavyowasikia hatujui kinachoendelea hadi sasa,” alisema abiria mwingine aliyejitambulisha kwa jina la Paulo.
Mabaharia wa meli hiyo walilazimika kutumia mitungi 11 kuzima moto huo na kufanikiwa kuuzima moto huo baada ya muda wa dakika 15.
Mkurugenzi wa Mamlaka ya Usafiri Baharini Zanzibar, Haji Vuai, amethibitisha kutokea kwa tukio hilo na tayari maafisa ya Mamlaka hiyo wameanza kuchunguza tukio hilo.
Alisema tukio hilo lilitokea majira ya saa 6:40 usiku na inaaminika chanzo cha moto huo ni sigara iliyotupwa na abiria asiyefahamika.
Hata hivyo alisema mabaharia waliokuwemo kwenye meli hiyo waliweza kuuzima, lakini baadhi ya mali zimeungua na nyingine kutupwa baharini wakati wa kuzima moto huo.
Alisema mtu mmoja amejeruhiwa mkononi alipojikata kwa chuma wakati wa harakati za kuokoa mizigo yake.
Afisa huyo alisema hadi jana mchana alikuwa bado hajapokea ripoti rasmi ya nahodha wa chombo hicho, ili iweze kufanyiwa kazi.
Nahodha wa meli hiyo, Sabini Morris, aliendelea na safari baada ya moto huo kuzimwa na meli hiyo ilitarajiwa kurejea tena Zanzibar jana jioni.
“Chanzo cha matatizo yaliyojitokeza sio hitilafu za meli ndio maana tumeiruhusu iendelee na safari baada ya moto huo kuzimwa”, alisema Mkurugenzi huyo.
CHANZO: NIPASHE
0 Comments