Aliyekuwa Mtangazaji wa Shirika la Utangazaji Tanzania (TBC), Jerry Murro (30), amedai mahakamani kwamba hakutenda makosa ya kula njama wala kuomba rushwa ya Sh. Milioni 10, kama anavyoshtakiwa bali zilikuwa njama za baadhi ya askari polisi wanamkandamiza ili kumpotezea maisha yake.
Kadhalika, alidai kuwa kutokana na kesi hiyo inayoendelea mahakamani hapo ambayo amekandamizwa na polisi wanaomchukia kwa kuibua matukio ya rushwa na ubadhilifu nchini, imesababisha apoteze ajira yake TBC, kufukuzwa kwenye nyumba ya kupanga, kukosa zawadi ya dola 4,000 za Marekani ambazo alipata tuzo ya Baraza la Habari Tanzania (MCT), pamoja na kufukuzwa kujiunga na masomo ya Chuo Kikuu cha Tumaini.
Muro alitoa madai hayo jana mbele ya Hakimu Mkazi, Frank Moshi, anayesikiliza kesi hiyo katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, jijini Dar es Salaam.
Akiongozwa na wakili wa utetezi Richard Rweyongeza, Muro ambaye ni shahidi wa kwanza wa upande wa huo, alidai kuwa kesi iliyopo mahakamani dhidi yake ni ya kukandamizwa na baadhi ya askari polisi ambao wamechukizwa na majukumu yake ya kufichua maovu mbele ya jamii ikiwemo kwa askari wa usalama barabarani na baadhi ya vigogo wa serikali.
“Kuna askari mmoja kati ya wale waliokuja kunikamata alinieleza ukweli kwamba walitumwa wanikamate na nikipokea rushwa lakini wamenisaidia wamenikamata kwa tuhuma za kuomba rushwa… Nilielewa moja kwa moja kwamba kuna baadhi ya polisi wameamua kuniangamiza kwa kunipotezea maisha katika sakata hili ambalo sijui mwanzo wake wala mwisho wake” alidai Muro.
CHANZO: NIPASHE