Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu jana iliahirisha kesi ya wizi dhidi ya watu wanne wanaoshtakiwa kwa kosa la kumuibia Josephine Mushumbuzi mkoba ukiwa na mali ya Sh. milion 1.1.
Josephine, ni mchumba wa Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Dk. Willibrod Slaa.
Kesi hiyo iliahirishwa mbele ya Hakimu Mkazi, Frank Moshi hadi Septemba 5, mwaka huu baada ya Wakili wa Serikali, Cecilia Mkonongo kuieleza mahakama kuwa upelelezi katika kesi hiyo bado haujakamilika.
Washtakiwa hao ni mfanybiashara Getis Mtuli (34) na mwendesha pikipiki Salum Mpanda (29), Gake Mwita (39) na Charles Steven (29) ambao walisomewa mashtaka yao mbele ya mahakimu watatu tofauti. 
Awali ilidaiwa kuwa Mtuli, Mwita, Mpanda na Steven wanadaiwa kula njama ya kutenda kosa la unyang'anyi wa kutumia silaha.
Iliendelea kudaiwa kuwa, Julai 13, mwaka huu, kati ya Suma JKT na Barabara ya Ali Hassan Mwinyi, washtakiwa waliiba mkoba, simu za mkononi aina ya nokia na kadi mbalimbali za benki.

Pia walidaiwa kuiba kamera moja ya digito, vitambulisho mbalimbali, leseni ya gari clasi D na Sh. 50,000 vyote vikiwa na thamani ya Sh.1, 190,000 mali ya Mushumbuzi.
Ilidaiwa kuwa kabla au baada ya kutenda kosa hilo la wizi washtakiwa walimtishia kumuua Mushumbuzi kwa bastola pamoja na shoka ili kufanikisha kutenda kosa hilo kwa urahisi.
Washtakiwa walikana mashtaka hayo. Hata hivyo, mahakama ilisema mashtaka yanayowakabili washtakiwa hayana dhamana ambapo kesi hiyo ilipangwa kutajwa Septemba 5, mwaka huu.
CHANZO: NIPASHE