Bendi maarufu nchini African Stars `Twanga Pepeta, itatumbuiza katika onyesho maalum ijulikanalo kama ‘Konyagi Iddi Pili Show’ ambalo limepamgwa kufanyika kwenye ukumbi wa TCC Club, Chang’ombe, Temeke siku ya Iddi Pili.
Mratibu wa onyesho hilo, Joseph Kapinga, amesema onyesho hilo limeandaliwa na Bob Entertainment chini ya udhamini wa kinywaji cha Konyagi.
Mkurugenzi wa Twanga, Asha Baraka, amesema kuwa onyesho hilo litatumika kutangaza albamu yao mpya itakayotambulishwa baadaye mwaka huu.
Nyimbo zilizomo kwenye albamu hiyo mpya ni pamoja na ‘Kauli’, ‘Kiapo cha Mapenzi’, ‘Umenivika Umaskini’, ‘Mtoto wa Mwisho’, ‘Dunia Daraja’ na ‘Penzi la Shemeji’. 
Kapinga alisema kuwa onyesho la TCC pia litatumika kumtambulisha ‘Kimwana wa Twanga Pepeta 2011’, Mary Khamis ambaye amejiunga na bendi hiyo kuchukua nafasi ya mnenguaji Aisha Madinda aliyetimkia katika bendi ya Extra Bongo.
Mbali na kimwana huyo, wanenguaji wengine nyota ni pamoja na Abdillahi Zungu, Fasha Sunday, Beatrice Mwangosi na Lillian Internet.
Pia Twanga Pepeta litatumbuiza siku ya Iddi Mosi Kwenye Ukumbi wa Mango Garden, Kinondoni na Iddi Tatu katika ukumbi wa Habours Club, Kurasini