Watu zaidi ya milioni mbili hawana umeme na kwa uchache wanane wamekufa wakati kimbunga Irene kilipopiga kanda ya mashariki ya Marekani.

Kimbunga hicho kimepungua kasi tangu kufika mwambao lakini hata hivo kinatarajiwa kuleta uharibifu mkubwa, hasa kwa sababu ya mafuriko.

Kimbunga hicho kiitwacho Irene kinafwata mkondo uliotabiriwa, kutoka kusini kuelekea kaskazini mwa kanda ya mashariki.

Kimeshamwaga mvua zaidi ya thuluthi ya mita katika sehemu fulani, na kuna ripoti kuwa mawimbi yamefumka kufika urefu wa karibu mita tatu.

Kinatarajiwa kupiga Philadelphia, Boston pamoja na mji wa New York, ambako wakaazi zaidi ya elfu 20 tayari wameshapoteza umeme kwa sababu ya upepo mkali.

Meya wa New York, Michael Bloomberg amefunga reli za chini kwa chini, na amewaomba wakaazi wasitoke nje hadi dhoruba ikishapita.

Wasiwasi mkubwa ni juu ya Mto Hudson usije ukajaa maji na kufurika katika mitaa ya Manhattan pamoja na Wall Street, mtaa wa masoko ya fedha.

Rais Obama amefupisha likizo yake ili kusimamia shughuli za serikali za kupambana na dhoruba hiyo.

Anataka kuepuka makosa yaliyofanywa wakati wa kimbunga Katrina, miaka 6 iliyopita, ambapo serikali ilichelewa kuchukua hatua.