Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ) imesema vita dhidi ya dawa za kulevya Zanzibar, haitafanikiwa iwapo wafanyabiashara wakubwa wanaoingiza dawa hizo wataendelea kuogopwa na vyombo vya dola.
Waziri wa Nchi katika Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais, Mohammed Aboud Mohammed alisema Jeshi la Polisi lifanye kazi kwa kuwachukulia hatua wahalifu bila kujali nafasi zao katika jamii.
Alikuwa anazungumza na makamanda wa Jeshi la Polisi na Idara ya Uhamiaji Zanzibar mjini hapa walioshiriki katika mkutano wa kujadili mpango wa kupambana na uhalifu Zanzibar juzi.
Alisema vitendo vya uhalifu vimekuwa vikikongezeka kwa kasi Zanzibar kutokana na udhaifu unaofanywa na vyombo vya Ulinzi katika kusimamia sheria na kusababisha uhalifu kuongezeka ikiwemo vitendo vya utapeli.
Alisema kwamba pamoja na Jeshi la Polisi kuwakamata watu wanaojishughulisha na biashara haramu ya dawa za kulevya bado hali sio nzuri kutokan na biashara hiyo kuendelea kuenea na kuathiri vijana Zanzibar.
Waziri Aboud alisema mwelekeo wa kesi za dawa za kulevya Zanzibar sio mzuri na kutoa mfano wa sampuli ya ushahidi wa kesi zilivyobadilika na kuwa seruji baada ya kufikishwa katika Ofisi ya mkemia mkuu wa Serikali na kusababisha washitakiwa kuachiwa huru na Mahakama.
Alisema haiwezekani mtu asafiri hadi Brazil na baadae ameze saruji tumboni, "lakini baadaye tunaambiwa sio dawa za kulevya saruji tuwe waadilifu katika kusimamia sheria.”
Waziri Aboud alisema kwamba sheria lazima zisimamiwe kwa vitendo na kuwataka polisi kutekeleza majukumu yao na kuwachukulia hatua wahalifu kwa mujibu wa sheria za nchi.
Waziri Aboud alisema kwamba katika kupambana na vitendo vya uhalifu wageni wanaoingia na kutoka Zanzibar watalazimika kukaguliwa maeneo ya uwanja wa ndege na bandari baada ya kuwepo malalamiko ya wageni kutoka Kenya, Uganda na India kufanyakazi kinyume na sheria.
Wakichangia katika Mkutano huo viongozi waandamizi wa Jeshi la Polisi Zanzibar waliomba serikali kuimarisha huduma za Uchunguzi katika Ofisi ya Mkemia mkuu kutokana na kukabiliwa na uchakavu wa vitendea kazi na kushindwa kutoa ripoti za uchunguzi kwa muda muafaka.
Mkuu wa upelelezi Wilaya ya Mjini Unguja, Haji Abdalla Haji alisema kwamba Ofisi ya Mkemia Mkuu inakabiliwa na tatizo la kuchelewesha matokeo ya uchunguzi wa sampuli ikiwemo za uchunguzi wa dawa za kulevya na kuathiri mwenendo wa kesi hizo.
Kamishina Msaidizi wa Polisi Zanzibar (SACP) Juma Yussuf alisema wakati umefika askari Polisi waruhusiwe kukagua hati za kusafiria pale wanapomtilia shaka abiria wakati wa kuingia na kutoka katika viwanja vya ndege na maeneo ya badarini.
Alisema kwamba iwapo Idara ya Uhamiaji Zanzibar wataondoa urasimu huo mafanikio makubwa yatapatikana katika kuwatafuta wafanyabiashara wanaoingiza dawa za kulevya Zanzibar.
CHANZO: NIPASHE JUMAPILI
0 Comments