Raia mmoja wa Afrika Kusini aliamka akajikuta yupo kwenye chumba cha kuhifadhia maiti mwishoni mwa juma, na akaanza kupiga kelele akitaka atolewe- akiwatisha wahudumu wakidhani ni mzimu.
Familia yake ilidhani amekufa baada ya kushindwa kumwamsha Jumamosi usiku na kuwasiliana na ofisi moja yenye vyumba vya kuhifadhia maiti ya mtu binafsi katika kijiji kimoja mjini Eastern Cape.
Alikuwepo kwenye chumba hicho kwa muda wa saa 24, msemaji wa idara ya afya mjini humo aliliambia shirika la habari la Sapa.
Wahudumu hao baadae walirejea na kupiga simu kuita gari la wagonjwa.
Mtu huyo ambaye jina lake limehifadhiwa, alitibiwa hospitalini kwa kukosa maji mwilini.
Msemaji wa idara ya afya ya Eastern Cape Sizwe Kupelo alisema, "Daktari walimfanyia uchunguzi na kuona kuwa anaendelea uzuri."
"Hakuhitaji matibabu ya ziada."
Bw Kupelo alisema mtu huyo aliamka saa tisa za Afrika Mashariki siku ya Jumapili, akitaka kutolewa kwenye chumba hicho chenye baridi kali kwenye kijiji cha Libode, na kuwatisha wahudumu waliokuwa zamu.
Bw Kupelo alisema, "Mwanzo watu hao walikimbia kwa kasi."
Maafisa wameusihi umma kuwasiliana na madaktari au wanaotoa huduma za dharura ili waweze kumtangaza mtu kufariki dunia kabla ya kuwaita wahudumu wa vyumba vya kuhifadhi maiti.
Bw Kupelo alisema, "Unaanza kujiuliza ni watu wengine wangapi waliokufa kwa namna hiyo katika chumba cha kuhifadhia maiti."
0 Comments