Utafiti mmoja wa kisayansi umesema, chombo ambacho ni rahisi kubebeka na chenye bei nafuu cha kupimia damu kinaweza kuleta mafanikio mapya katika kubaini ugonjwa hasa katika maeneo ya vijijini.
Kulingana na utafiti uliofanywa na jarida la Nature Medicine, chombo hicho kiitwacho mChip kina ukubwa wa kadi ya benki na huweza kutambua maradhi katika kipindi cha dakika chache tu.
Upimaji wa sampuli za awali za maradhi kama ukimwi na kaswende nchini Rwanda zilionyesha takriban asilimia 100 kuwa sahihi.

Kifaa hicho kilichotengenezwa Marekani kitagharibu dola moja ya kimarekani.
Gharama yake ni ndogo zaidi ukilinganisha na upimaji unaofanyika kwenye maabara ambao ndio unaotumika kwa sasa.
Kibanzi au chip hiyo ina maeneo 10 ya kutambua, na kinaweza kupima ugonjwa zaidi ya moja kwa damu kidogo tu inayotokana kwa kujichoma na sindano ndogo.
Majibu yanaweza kuonekana kwa macho tu au kwa chombo cha kutambua chenye bei nafuu.
Samuel Sia, Profesa kutoka chuo kikuu cha Columbia ambaye ndiye kiongozi wa uundwaji wa kibanzi hicho alisema, " Wazo kuu lilikuwa ni kuweza kupima maradhi mengi na iweze kuwafikia wagonjwa popote duniani, badala ya kuwalazimisha kwenda kwenye zahanati kutoa damu na kusuburi majibu kwa siku kadhaa."
Upimaji mwingi uliofanywa kwa sampuli za awali za kifaa hicho zilifanyika mjini Kigali, Rwanda.
Zilionyesha kuwa sahihi kwa asilimia 95 baada ya kupimwa kwa virusi vya ukimwi na sahihi kwa asilimia 76 baada ya kupima kaswende.
Watafiti wana matumaini ya kutumia mChip kujaribu kuongeza uwezekano wa kupima maradhi yanayoambukizwa kwa njia ya kujamiiana kwa wajawazito, hasa barani Afrika.
Aina nyingine ya kibanzi hicho nacho kimeundwa kupima saratani ya kibofu.