Kocha wa zamani wa timu ya taifa, Taifa Stars, Marcio Maximo(Pichani juu) ambaye aliondoka nchini akidai kuwa na ofa za kufundisha klabu za Afrika Kusini na Israeli hajapata timu mpaka sasa, kwa mujibu wa uchunguzi.
Maximo, 49, aliondoka nchini katikati ya mwaka jana baada ya kumaliza mkataba wa miaka mitatu na shirikisho la soka, TFF, na nafasi yake kuchukuliwa na Mdenmark Jan Poulsen.
Kocha huyo aliondoka akiwa amewagawa wapenzi wa soka nchini baadhi wakimshutumu kwa kufifisha kiwango cha Taifa Stars kutokana na kushindwa kutengeneza kikosi cha kudumu wala kuleta ubingwa, wengine wakimuona mwalimu aliyeweka misingi ya maendeleo.

Maximo aliondoka katikati ya mwaka jana akidai kuwa na ofa za kufundisha Orlando Pirates na Hapoel Tel Aviv, miongoni mwa nafasi nyingi tofauti.
Lakini kwa mujibu wa uchunguzi uliofanywa katika mtandao wa kompyuta, taarifa za mwishoni zaidi za kikazi za kocha huyo ni kufundisha Taifa Stars.
Haikuelezwa kilichotokea katika mipango ya Maximo kufundisha mabingwa wa vikombe vitatu vikubwa msimu uliopita wa Afrika Kusini Pirates wala washindi wa pili wa ligi kuu ya Israel hao.
Kabla ya kuja kufundisha Stars kupitia msaada wa kiufundi wa serikali ya Brazili, Maximo alikuwa mmoja wa benchi la ufundi la kikosi cha Brazili cha under-17 na under-20 kuanzia mwaka 1992 mpaka 1993.
Timu hizo zilijumuisha wachezaji nyota wa baadaye kama Ronaldo na Ronaldinho.
Alikuwa mkurugenzi wa ufundi wa Visiwa vya Grand Cayman kwa miaka mitatu wakati alipokataa ofa ya nyongeza ya miaka 10 na kujiunga na klabu ya Scotland ya Livingston Juni 5, 2003.
Hata hivyo, mambo hayakwenda vizuri na baada ya mechi tisa (kushinda 3, sare 3 na vipigo vitatu) alijiuzulu Oktoba 14.
Ndipo Juni 29, 2006, Maximo alipoteuliwa kuwa kocha wa Tanzania na kuisaidia kufuzu kwa fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika kwa wachezaji wa ligi za nyumbani, CHAN, zilizofanyika Ivory Coast kati ya Februari 22 mpaka Machi 8, 2009.
Maximo aliongeza mkataba wake na TFF kwa mwaka mmoja mpaka Julai 2010 lakini katika miaka mitatu hiyo timu haikuwa na mafanikio mpaka ilipochukuliwa na Poulsen na kutwaa angalau Kombe la Chalenji miezi michache baadaye.