Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ) imesema inatarajia kutumia Sh Bilioni 9.9 kuwahudumia viongozi wake wakiwemo wastaafu kwa kuwalipa pensheni na safari za nje katika Mwaka huu Fedha.
Hayo yameelezwa na Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Fedha na Uchumi Omar Yussuf Mzee, Wakati akifunga mjadala wa Bajeti yake katika Kikao cha Baraza la Wawakilishi kinachoendelea katika mji wa Chukwani mjini Zanzibar.
Alisema kwamba kati ya fedha hizo Sh Bilioni 4.4 zitatumika kwa Safari za nje kwa viongozi wa kitaifa wa Serikali pamoja na viongozi wake wastaafu Zanzibar.
Aliwataja viongozi watakao nufaika na kasma hiyo kuwa ni marais wastaafu ambao ni Ali Hassan Mwinyi, Dk Salmin Amour Juma, Amani Abeid Karume, naa Aboud Jumbe Mwinyi.
Aidha aliwataja mawaziri kiongozi wastaafu kuwa ni Ramadhani Haji Faki, Dk Mohammed Gharib Bilali na Waziri wa Mambo ya ndani Shamsi Vuai Nahodha.
Aidha alisema fedha hizo zimetengwa pia kwa ajili ya malipo ya pensheni mbali na kutumika kwa gharama za safari za nje kwa viongozi hao, lakini hakusema viongozi hao wastaafu Zanzibar wamekuwa wakilipwa kiwango gani cha fedha kila mwezi.
Waziri Omar ametoa ufafanuzi huo baada ya Ismail Jussa Ladhu (Mji Mkongwe) kulalamika kwamba Sh Bilioni 4.5 zilizotengwa kwa Safari ni kiwango kikubwa kutokana na Zanzibar kukabiliwa na matatizo mbali mbali ya huduma za jamii kwa wananchi wake
Hata hivyo, Waziri Omar alisema kiwango hicho cha fedha ni cha kawaida kwa sababu pia kitatumiwa na viongozi wa kitaifa serikalini akiwemo Rais wa Zanzibar, Dk. Ali Mohammed na makamu wake Maalim Seif Sharif Hamad, na Balozi Seif Ali Iddi.
Kuhusu Kamati ya Pamoja ya Fedha ya Serikali ya Muungano na Zanzibar (JFC) alisema Kamati hiyo tayari imekamilisha ripoti yake na kinachosubiriwa ni Mapendekezo ya Serikali ya Muuungano baada ya Baraza la Mapinduzi kukamilisha kazi ya kupitia ripoti hiyo na kutoa mapendekezo yake.
Alisema SMZ tayari imeshapokea ripoti na kutoa mapendekezo yake, lakini Serikali ya Jamhuri ya Mungano bado haijakamilisha kupitia ripoti hiyo na kutoa mapendekezo yake.
Waziri huyo alisema kwamba kila upande wa Muungano umetakiwa kutoa mapendekezo katika ripoti hiyo kuhusu utaratibu wa kufungua akaunti ya pamoja na utaratibu utakaotumika katika kuchangia mfuko wa pamoja wa mapato kutoka katika vyanzo vya mapato vya Muungano.
Hata hivyo, alisema kweli Tume hiyo ina muda mrefu tangu iipoundwa lakini aliwataka wajumbe waendelee kuwa wastahamilivu wakati serikali zikiiendelea kukamilisha hatua iliyobakia katika suala hilo.
Awali Wajumbe Baraza hilo walitaka kujua Kamati hiyo imefikia hatua gani katika kuweka mpango mpya wa mgao wa mapato yatakanayo na vyanzo mbali mbali vya Mapato ya Muungano wa Tanganyika Zanzibar.
0 Comments