MBUNGE wa Ludewa, Deo Filikunjombe (CCM), ameliambia Bunge kwamba umasikini wa Watanzania unatengenezwa .

Mbunge huyo alisema hayo wakati akichangia mjadala wa bajeti ya Wizara ya Viwanda na Biashara kwa mwaka wa fedha 2011/12.

Aidha Filikunjombe alisema watendaji si makini na hawajali maslahi ya nchi. Mbunge huyo alisema hayo huku akitoa mfano wa barua aliyodai imeandikwa na Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini, David Jairo kwenda kwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Viwanda, Biashara na Masoko kumtaka asitishe miradi ya Liganga na Mchuchuma.

Akichangia , Filikunjombe alisema katika nchi yoyote duniani kama hakuna viwanda hata maendeleo ya wananchi wake ni dhaifu.

Alisema watendaji wa Serikali ndiyo wanaochangia kurudisha nyuma maendeleo ya Watanzania kwani pamoja na usemi wa kwamba kupanga ni kuchagua, watendaji hao wamechagua kurudisha nyuma maendeleo ya nchi.

Mbunge huyo alilionesha Bunge barua hiyo, iliyoandikwa Machi 21, mwaka huu ikitoka kwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini, David Jairo kwenda kwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Viwanda, Biashara na Masoko, Joyce Mapunjo.

Hata hivyo mbunge huyo hakuisoma barua hiyo kwa wabunge bali alizungumzia maudhui ya barua hiyo na kusema, kuwa inamtaka Mapunjo kusitisha miradi tajwa.

“Haiwezekani kiongozi mkubwa kwenye wizara kama hiyo kusimamisha miradi mikubwa kama hiyo ambayo ina manufaa kwa wananchi, sasa hapa tunakwenda mbele au kurudi nyuma?” Alihoji Mbunge huyo.

Alihoji kama mtendaji mkubwa kama huyo anakwamisha miradi kama hiyo, nchi itaendeleaje?

Alisema suala hilo linaonesha jinsi gani Serikali haitekelezi wajibu wake ipasavyo kwa maslahi ya wananchi.

Hata hivyo Mbunge huyo alisema ameiwasilisha barua hiyo kwa Waziri Mkuu kama kielelezo cha aliyosema.

Akichangia mjadala huo Mbunge wa Viti Maalumu, Naomi Kaihula (Chadema), alisema Shirika la Maendeleo nchini (NDC), lazima liwezeshwe ili lifanye kazi ya maendeleo, kwani kwa kulipa fedha kidogo tofauti na zilizoombwa ni kulikwamisha.

Mbunge wa Mkanyageni, Habib Mnyaa (CUF), alihoji kwa nini miradi mingi nchini imepewa wawekezaji kutoka China.

Alisema sio busara wala haki kwa Serikali kutoa zabuni za miradi mingi nchini kufanywa na Wachina na kutoa mfano wa miradi hiyo kama ile ya Liganga, Mchuchuma na Kiwira na kusema iko siku nchi inaweza kupishana lugha wawekezaji hao wakiigeuka nchi.