Mkuu wa zamani wa Jeshi la Zimbabwe Solomon Mujuru amefariki dunia kwa moto katika shamba lake, taarifa rasmi zimeifikia BBC.
Bw Mujuru mwenye umri wa miaka 62, alikuwa mwanasiasa mwandamizi na mume wa Makamu wa Rais wa Zimbabwe Joice Mujuru.
Wachambuzi wanasema kifo chake huenda kitazidisha mkanganyiko kwenye chama cha Rais Mugabe kuhusu nani atakayemrithi kiongozi huyo mwenye umri wa miaka 87.
Akijulikana kama Rex Nhongo wakati wa vita vya msituni, alikuwa mkurugenzi wa vikosi vya Muganbe wakati wa vita vya uhuru miaka ya 1970s’.
Afisa mmoja ameiambia BBC kuwa Jenerali Mujuru alikufa kwa moto uliotokea katika nyumba yake ya shambani katika eneo la Beatrice, kilometa 80 (maili 50) kusini mwa mji mkuu Harare asubuhi ya Jumanne.
Haijulikani iwapo alikuwa peke yake wakati huo au kama alipewa ulinzi wa jeshi.
Rais Mugabe anatarajiwa kutoa tamko rasmi kuthibitisha kifo cha Jenerali Mujuru baadaye leo kwa mujibu wa itifaki za chama cha Zanu-PF.
Mwandishi wa BBC Brian Hungwe mjini Harare anasema Jenerali Mujuru alikuwa mwanachama mwandamizi wa chama cha Zanu-PF na anaelezwa kuwa alikuwa mwenye msimamo wa kadri.
Alikuwa mpanga mikakati na kusemekana akiwa na ushawishi mkubwa wa kuweka viongozi wenye nguvu katika siasa za Zanu-PF , anasema.
Kifo chake kimeacha pengo na kumuuacha mkewe bila nguzo ambaye ni mmoja kati ya makamu wawili wa Rais, wachambuzi wanasema.
Wakati wa vita dhidi ya utawala wa Rhodesia katika miaka ya 1970s, Jenerali Mujuru aliongoza mapambano ya silaha pamoja na marehemu Josiah Tongogora.
Mwandishi wa BBC anasema alikuwa Jenerali Mujuru aliyewahamasha wapigania uhuru wa Msumbiji wakati wa mgogoro kumkubali Bw Mugabe kama kiongozi wa vikosi vya vuguvugu la waasi wa Zanla baada ya kuachiliwa kutoka kizuizini mwaka 1974.
Wakati wa uhuru mwaka 1980 aliongoza kikosi cha jeshi kabla ya kustaafu na kuingia katika biashara miaka 10 baadaye.
Mwandishi wetu anasema akiwa kiongozi wa wapigania ukombozi dhidi ya utawala wa kikoloni, Jenerali Mujuru anatarajiwa kuzikwa kwa heshma ya kitaifa, katika makaburi ya mashujaa baadaye wiki hii.
0 Comments