Shirika la kimataifa la kutetea haki za kibinadamu Human Rights Watch limezindua ripoti mpya ambayo imewashutumu wale wote wanaohusika katika vita nchini Somalia kwa ukiukaji mkubwa wa haki za kibinadamu.

Shirika hilo linadai kuwa ukiukaji huo wa haki za kibinadamu umechangia pakubwa katika mkasa unaolikabili taifa hilo.

Ripoti ya shirika hilo yenye kichwa "You Don't Know Who to Blame" au hujui wa kumlaumu inasema kuwa pande zote katika mzozo wa Somalia ni sharti zikomeshe unyanyasaji wa raia na kuwaruhusu kupokea msaada.
Katika repoti hiyo, HRW linasema raia wa kawaida ndio wanaoteseka zaidi kwani pande zote hapa ikiwa ni serikali ya mpito, vikosi vya jeshi la kulinda amani vya Umoja wa Afrika na kundi la wapiganaji la Al shabaab linawatesa.

Shirika hilo limeongeza kuwa kila siku wapiganaji wa Al shabaab wanawatendea ukatili raia, kwa kuwazuia kuondoka maeneo ambayo wanayadhibiti, kwa kuwa inawatumia kama kinga dhidi ya mashambulizi kutoka wanajeshi wa Umoja wa Afrika na wale wa serikali ya mpito ya somalia.


Shirika hilo pia limelaumu serikali ya Kenya kwa kushindwa kulinda haki za wakimbizi wanaoingia nchini humo.

HRW imesema kuwa polisi wa Kenya wanawahangaisha sana wakimbizi wanaoingia kutoka Somalia.

Ripoti hiyo imependekeza kuwa baraza la usalama la umoja wa mataifa libuni tume ya kuchunguza ukiukaji wa haki za kibinadamu unaoendelea nchini Somalia na kuwachukulia hatua wote wanaohusika.

Shirika hilo pia limetaka serikali ya mpito nchini humo na kundi la Al shabaa liache kuwatumia raia kama kinga wakati wa vita.

Pia linataka kundi la Al shabaab liruhusu mashirika ya kutoa misaada yakiwemo yale ya Umoja wa Mataifa kusambaza misaada kwa wanaokabiliwa na njaa.

Kwa upande mwengine HRW imeitaka Kenya ifungue kambi ya wakimbizi ya Ifo II ilioko kaskazini mwa nchi hiyo kama njia moja ya kumaliza msongamano kwenye kambi zinazowahifadhi wakimbizi kwa sasa.

Shirika hilo pia limetaka jeshi la Kenya na lile la Ethiopia lihakikishe kuwa harakati zao za kulinda sehemu za mipakani zinafuata sheria na kuwa raia wa wasio na hatia kutoka Somalia hawa dhalalishwa au kuteswa.