JAJI Mkuu mstaafu, Augustino Ramadhani amesema kwamba amewahi kushurutishwa kutoa hukumu na baadhi ya viongozi wa Serikali wakati wa utendaji kazi wake.

Jaji Ramadhani aliyasema hayo wakati akitoa mada juu ya Utii wa Sheria Bila Shuruti wakati wa uzinduzi wa maadhimisho ya miaka 50 ya Chuo cha Polisi Dar es Salaam yanayoenda sambamba na maadhimisho ya miaka 50 ya Uhuru.

Alisema wakati akiwa anafanya kazi Zanzibar, kuna mwalimu mmoja alimchapa mwanafunzi ambaye kesho yake alifariki na kutakiwa kumkamata na kumhukumu kitu ambacho alisema alipingana nacho.

Alisema aliona kwamba siyo adhabu ya mwalimu iliyomsababishia mtoto huyo kifo isipokuwa kwa kuwa mzazi wake alikuwa akifanya kazi serikalini alishinikiza mwalimu huyo kukamatwa, jambo ambalo alipingana nalo.

“Viongozi wanapaswa kutenda haki mana wakati mwingine sheria inavunjwa kwa kulindana, ni lazima tuambiane ukweli kwa manufaa ya miaka 50 ijayo,” alisema Jaji Mkuu mstaafu.

Alisema pamoja na kwamba sheria inaeleza wazi kwamba Jaji anapaswa kulindwa, lakini baada ya yeye kustaafu, siku iliyofuata alinyang’anywa ulinzi.

“Siku hiyo walinifungulia nikatoka na wakati narudi sikuwakuta ikanibidi tutafute Wamasai kwa ajili ya kutusaidia ulinzi, sasa hii nilifanyiwa mimi ambaye Oktoba nilimuapisha Rais, je, kwa mtu wa kawaida inakuwaje?” Alihoji.

Alisema jambo hilo lilipotokea hakumueleza mtu yeyote ila kwa kuwa inatakiwa utii wa sheria ameamua kuliweka wazi.