WAZIRI wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Shamsi Vuai Nahodha ametoa wiki mbili kwa wageni wanaofanya kazi nchini bila kuwa na vibali vya ukazi, wajisalimishe Idara ya Uhamiaji ili wasaidiwe kuondoka nchini ama kuelekezwa namna ya kuvipata vibali hivyo.
Kwa mujibu wa taarifa ya Wizara hiyo iliyotolewa jana kwa vyombo vya habari Dar es Salaam jana, Nahodha pia amewataka wanaowaajiri wageni hao kuwa na vibali hivyo, vinginevyo watachukuliwa hatua ikiwemo kufikishwa katika vyombo vya sheria.
Alitoa maagizo hayo jana wakati wa mazungumzo yake na viongozi wa Idara ya Uhamiaji ambao pamoja na mambo mengine, amewaagiza kusimamia kikamilifu zoezi hilo litakaloendeshwa nchi nzima.
Alisema katika siku za hivi karibuni kumekuwepo na taarifa mbalimbali zinazotolewa katika vyombo vya habari na zingine ofisini kwake kuhusu uwepo wa wageni hao wanaofanya kazi katika maeneo mbalimbali ya nchi bila ya kuwa na vibali vya ukazi.
“Ni lengo, vyema niwakumbushe tena waajiri na wageni wanaoingia nchini kuwa lengo la kuomba ajira linafuatana na sheria za nchi yetu, mgeni yeyote haruhusiwi kuomba ajira kama hana kibali cha ukazi kinachotolewa na Idara ya Uhamiaji,” alisema Nahodha.
Waziri huyo alisema baada ya wiki mbili kumalizika, wageni wote wanaofanya kazi bila ya kibali cha waajiri watakamatwa na watatangazwa majina yao.
Aidha, alisema vibali vya ukazi ni pamoja na kibali cha ukazi Daraja “A” kinachotolewa kwa wawekezaji wakubwa wanaoingia nchini kuwekeza katika kampuni, viwanda, uvuvi, madini na usafishaji alivyoeleza hutolewa baada ya muombaji kutimiza masharti yanayohusu
masuala la uwekezaji.
Pia kibali cha Daraja “C” hutolewa kwa wageni wanaoomba ajira katika viwanda, kampuni binafsi, shughuli za uvuvi, machimbo, usafirishaji na bendi za muziki ambavyo ili muombaji apewe, anapaswa kuomba kibali cha kufanya kazi kutoka Wizara ya Kazi na Ajira.
Alisema kibali cha “C” kinatolewa kwa Wamisionari, watafiti na wanafunzi, baada ya kuomba vibali vya kuwawezesha kufanya shughuli zao nchini.

0 Comments