Rais wa Eritrea -Isaias Afeworki(pichani) jana alitarajiwa kuanza ziara rasmi ya siku tatu nchini Uganda.
Ziara hiyo inafanyika wakati Eritrea imeomba kurejesha tena uanachama wake katika shirika la maendeleo la nchi za pembe ya Afrika IGAD.Huenda Rais Aferworki na mwenyeji wake Yoweri Museveni wakaangazia zaidi suala hilo kwenye mkutano wao.
Baadhi ya wanachama wa IGAD wamependekeza Eritrea iwekewe vikwazo kwa kuwa inaunga mkono wapiganaji wa Al Shabaab wanaoipinga serikali ya mpito nchini Somalia.
Rais Afeworki hana mazoea kutembelea nchi za kigeni na wadadisi wa masuala ya kidiplomasia wanasema huenda ni juhudi za kujenga upya uhusiano kati ya serikali yake na nchi jirani.
Mwezi uliopita, Eritrea iliomba kujiunga tena na shirika la maendeleo la Afrika Mashariki Igad, baada ya kujitoa kama mwanachama mwaka wa 2006.
Katibu mtendaji wa Igad Mahboub Maalim alisema ombi hilo litajadiliwa na wanachama kabla nchi hiyo kuruhusiwa kujiunga tena.
Utawala mjini Asmara uliamua kufuta uanachama wake wa Igad baada ya mahasimu wao Ethiopia kutuma majeshi yake nchini Somalia kupambana na vikosi vya Umoja wa mahakama ya kiislamu wakati waliokuwa wanatawala sehemu kubwa ya kusini mwa nchi hiyo.
Mwezi uliopita Igad ilipendekeza kwa baraza la uslama la umoja wa mataifa liiwekee vikwazo serikali ya Eritrea kufuatia vitendo vyake vya kushirikiana na kundi la wapiganaji wa Al Shabaab wanaoipinga serikali ya mpito ya Somalia.
Mwandishi wa BBC mjini Kampala anasema huenda suala la mzozo unaoendelea nchini Somalia likawa hoja kwenye mkutano kati ya Rais Afeworki na mwenyeji wake Yoweri Museveni.
Tume maalum inayochunguza utekelezaji wa vikwazo vya kuingiza silaha nchini Somalia, hivi karibuni, ilidai kwenye ripoti yake kuwa Eritrea ilihusika na mpango wa kushambulia mkutano wa viongozi wa nchini wanachama wa Umoja wa Afrika uliofanyika mwezi Januari mwaka huu.
Ingawa mpango huo ulitibuliwa na vyombo vya usalama nchini Ethiopia, tume hiyo ilisema harakati za Eritrea za kuhujumu usalama katika eneo la Afrika Mashariki ikishirikiana na wanachama wa Al Shabaab zipo wazi.
Hata hivyo serikali ya Eritrea imekanusha madai hayo na badala yake kunyoshea mahasimu wao Ethiopia ambao wanasema ndio chanzo cha uvumi huo.
Uhusiano kati ya Eritrea na Ethiopia upo katika hali mbaya kufuatia mzozo wao kuhusu umiliki wa mji wa Badme uilioko kwenye mpaka wa nchi hizo mbili.
Licha ya mahakama ya kimataifa kuamua kuwa mji huo upo nchini Eritrea, utawala mjini Addis Ababa umekataa kutii amri ya mahakama hiyo.
0 Comments