Wizara ya Afrika Mashariki imeunda timu ya wataalam kwa ajili ya kuangalia mianya iliyopo katika sheria mbalimbali ambayo inaweza kutumiwa vibaya na wageni kinyume na matarajio ya utekelezaji wa itifaki ya Soko la Pamoja.
Waziri wa Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Samuel Sitta, alisema jana wakati akisoma hotuba yake ya bajeti ya wizara yake kwa mwaka 2011/2012.
Sitta alisema mapendekezo yaliyotolewa na tume hiyo ya wataalam yanafanyiwa kazi na serikali na kwamba timu hiyo itaendelea kuzipitia sheria katika maeneo mengine yaliyosalia katika mwaka 2011/2012. 
Alisema pamoja na tume hiyo kupitia katika maeneo hayo, pia kwenye hatua za awali imepitia sheria zinazoangaliwa na tume hiyo zinahusiana na uanzishwaji na uendeshaji wa shughuli za biashara, uwekezaji, ajira, uhamiaji, soko la mitaji na biashara ya huduma.
Pia alisema tayari tume hiyo imekwishapitia sheria zinazohusu uanzishaji wa makampuni, mikataba, ufilisi, majina ya biashara na uhamiaji na kupendekeza maeneo yanayopaswa kurekebishwa ili kutekeleza kuwezesha utekelezaji wa itifaki ya Soko la Pamoja.
Akisoma mamoni ya Kamati ya Bunge ya Mambo ya Nje, Ulinzi na Usalama kuhusu wizara hiyo, Betty Machangu, alisema ili kujipanga ipasavyo na kukabiliana na changamoto za uanzishwaji wa shirikisho la kisiasa walitaka kiwepo kitengo mahususi cha utafiti kitakachowezeshwa kwa kupewa raslimali sambamba na kupatiwa fedha za kufanyia tafiti mbalimbali.

Kwa upande wake kambi ya upinzani bungeni, ilitaka Sitta aeleze kwanini fungu la mafuta na vilainisho limeongezeka kwa kiasi kikubwa katika bajeti yake.
Alisema fungu hilo limeongezeka kutoka sh milioni 92.6 hadi sh bilioni 182 katika bajeti ya mwaka huu wa fedha. “Hata kama bei ya mafuta imepanda haiwezekani ongezeko liwe kubwa kiasi hiki,” alisema Mustafa Akunaay ambaye ni msemaji mkuu wa kambi hiyo kuhusiana na wizara hiyo.
CHANZO: NIPASHE