TIMU ya soka ya Taifa ya Tanzania ‘Taifa Stars’ inatarajiwa kuondoka Dar es Salaam leo kuelekea Khartoum, Sudan kwa ajili ya mchezo wa kirafiki na timu ya Taifa ya huko.

Ofisa Habari wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Boniface Wambura, alisema jana kuwa Stars itacheza ugenini Jumatano mchezo ambao upo katika tarehe inayotambuliwa na Shirikisho la Kimataifa la Mpira wa Miguu (Fifa).

Alisema kuwa wachezaji hao 14 wa Stars wataungana na wachezaji sita wa Yanga waliotangulia na timu yao juzi, ambapo jana Yanga ilitarajiwa kucheza mechi ya kirafiki na El Hillal ya Sudan.

“Wachezaji wa Yanga wataungana na wenzao kesho ( leo), kwa ajili ya maandalizi ya mechi,” alisema Wambura na kuongeza kuwa wachezaji hao hawatakuwepo kwenye kikosi cha Yanga kitakachocheza Jumanne na El Merreikh.



Wachezaji hao wa Stars waliopo na yanga ni Shaaban Kado, Shadrack Nsajigwa, Nadir Haroub, Chacha Marwa, Juma Seif na Godfrey Taita.

Julius Mrope yeye aliachwa katika kikosi cha Yanga kilichoondoka juzi, ambapo yupo katika kikosi cha Stars, wakati Nurdin Bakari ameachwa kwa sababu ni majeruhi.

Wachezaji wengine wanaotarajiwa kuondoka leo na timu zao katika mabano ni Shabani Dihile (JKT Ruvu), Aggrey Morris (Azam), Juma Jabu (Simba) na Juma Nyoso (Simba).

Shaaban Nditi (Mtibwa Sugar), Jabir Aziz (Azam), Soud Mohamed (Toto Africans), Salum Machaku (Simba), Julius Mrope (Yanga), Mrisho Ngassa (Azam), Hussein Javu (Mtibwa Sugar), John Bocco (Azam) na Thomas Ulimwengu (U23).