SHAMBULIO la risasi za moto lililofanywa na walinzi wa Kampuni ya Kichina dhidi ya wafanyakazi wa Kitanzania, limesababisha majeruhi saba.

Hatua hiyo imefanya Jeshi la Polisi Mkoa wa Rukwa, kushikilia raia wawili wa Kichina kwa tuhuma za kuwapiga risasi na kuwajeruhi wafanyakazi hao.

Wafanyakazi hao wa kampuni ya ujenzi wa barabara ya Hunan Construction Engineering Group East Africa Limited, inayojenga barabara kwa kiwango cha lami kutoka Kanazi hadi Kibaoni wilayani Nkasi, walipigwa risasi juzi asubuhi na kujeruhiwa na wengine kulazwa katika hospitali ya Serikali ya Mkoa wa Rukwa mjini hapa.

Inasemekana chanzo cha kupigwa risasi watu hao ni vurugu zilizozuka baina yao na raia hao wa China ambao ni Wancheng Utaha (46) na Hongdingalai (36) ambao sasa wanashikiliwa na polisi.

Wachina hao wanadaiwa kumkamata dereva aitwaye Shabani akiiba mafuta kutoka kwenye moja ya magari ya kampuni hiyo.

Baada ya kunaswa kwa dereva huyo, ambaye inadaiwa alikuwa akipelekwa ofisini kwa bosi wake, wenzake walipinga na kuwazuia walinzi hao, ndipo zikazuka vurugu kubwa kiasi ambacho kiliwalazimisha kufyatua risasi angani.

Pamoja na walinzi hao kufyatua risasi hizo, vurugu ziliendelea, kwani kundi la madereva wa kampuni hiyo, lilirusha mawe kuelekea kwa walinzi hao ndipo wakachukua uamuzi wa kufyatua risasi zikiwalenga miguuni na kuwajeruhi.



Kwa mujibu wa Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Rukwa, Isuto Mantage, watu watatu kati ya saba waliopigwa risasi na kulazwa katika hospitali hiyo, ni Rajabu Juma (28) ambaye ni dereva na mkazi wa kijiji cha Mpalamawe ambaye ilimpata mkononi.

Wengine ni Robert Kipaila (23) wa Mpalamawe pia aliyejeruhiwa kwenye paja la mguu na hali yake inaelezwa kuwa mbaya akihitaji upasuaji na wa tatu ni Britrick Wilbert (26) ambaye alijeruhiwa chini ya goti.

Kamanda Mantage aliwataja majeruhi wanne waliotibiwa kwenye hospitali teule ya wilaya ya Namanyere, Nkasi na kuruhusiwa kuwa ni Samwel Abidui (32) aliyepata jeraha kichwani lakini kwa kupigwa nondo wakati wa vurugu hizo, kabla risasi kufyatuliwa.

Aliwataja wengine ambao ni wakazi wa kijiji hicho ambao ni madereva wa magari na mitambo ya kampuni hiyo kuwa ni Bernard Eliusa (27), Mussa Elieza (22) na Ernest Kashuja (30) ambao walipata michubuko mwilini.

Kamanda Mantage alisema silaha aina bastola na risasi ambazo hakutaja idadi, zilikamatwa huku watuhumiwa hao wakiendelea kushikiliwa na watafikishwa mahakamani baada ya uchunguzi wa tukio hilo kukamilika, ili sheria ifuate mkondo wake.