MBUNGE wa Kigoma Kaskazini, Kabwe Zitto, amewaponda wabunge wanaosimama bungeni na kudai waongezwe mishahara na posho.

Zitto amesema, ni makosa mwa Mbunge hivi sasa kudai nyongeza hiyo kwa kuwa Taifa linakabiliwa na matatizo mengi ukiwemo upungufu wa umeme na upungufu wa fedha.

Ametoa msimamo huo bungeni mjini Dodoma wakati anachangia bajeti ya Wizara ya Afrika Mashariki kwa mwaka wa fedha 2011/ 2012 iliyowasilishwa leo.

Zitto amewataka wabunge wawe na mtazamo wa kiuongozi, waonyeshe wanaguswa na matatizo yanayowakabili Watanzania.

Wabunge walionekana kupingana na msimamo wa Zitto, yeye amesema hata kama wanampinga, hivi sasa ni makosa kutaka nyongeza ya mishahara na posho za wabunge.

Wakati anachangia bajeti ya Wizara hiyo, Zitto alisema, Watanzania wanapaswa waache kulalamika, sekta binafsi na wananchi waandaliwe watumie fursa za kiuchumi zilizopo katika Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC).

Mbunge huyo amesema, Tanzania ina fursa nzuri zaidi ya kibiashara miongoni mwa nchi wanachama wa EAC, wajipe moyo kuwa wanaweza kwa kuwa uwezo huo wanao.

“Kwa nini tusiseme kuwa tunaweza na tusijipe moyo kuwa tunaweza kufanya zaid? amehoji Mbunge huyo na kusisitiza kuwa, Tanzania ikitumia vizuri rasilimali zake, baada ya miaka michache, itakuwa na uchumi mkubwa zaidi miongoni mwa nchi wanachama wa EAC.

“Tujipe moyo tunaweza… najua Watanzania wanaogopa kuhusu ajira…tunachotakiwa kufanya ni nini, tuwaandae watu wetu” amesema Zitto na amehoji Watanzania wamendaliwa vipi kutumia fursa zilizopo katika nchi nyingine?

Mbunge wa Kigoma Mjini, Peter Serukamba, amesema, Tanzania ina nafasi kubwa zaidi ya kunufaika kiuchumi kulinganisha na nchi nyingine wanachama wa EAC kwa kuwa Mungu kaijalia rasilimali nyingi.

“Tufanye yote lakini tujikite zaidi katika uchumi na biashara” amesema Mbunge huyo na amesema, hayo yazingatiwe kwanza, shirikisho la kisiasa lisubiri.

“Mheshimiwa Mwenyekiti, Tanzania Mungu atupe nini, mimi nikisikia mnawasifu Wakenya ni kwa sababu tumeamua kujidharau…mimi naamini Watanzani tutakuwa giants” amesema Serukamba.

“Kwa hiyo kama nchi tujiandae, tuache kulalamika…tupo wengi kuliko wenzetu, tuanze culture (utamaduni) ya kufanya kazi…tuache visingizio” amesema Mbunge na kushauri kuwa vikwazo vya biashara viondolewe.

“Tuache kulalamika kama taifa kwa sababu tunaishi kwenye dunia moja, hatuishi kwenye kisiwa” amesema na kusisitiza kwamba, kwa kuwa Tanzania inahitaji kufanya biashara, Serikali iboreshe utaratibu wa viza.

Mbunge huyo Tanzania inapaswa kuuza nje bidhaa za viwandani badala ya mazao ghafi na pia ifanye tathmini ya sera zake za biashara.

Mbunge wa Viti Maalum, Mary Mwanjelwa amesema, ni kweli Watanzania wana kasumba ya uoga na kutofanya kazi, na kwamba, haya yanayofanywa sasa a EAC ni kwa ajili ya kizazi kijacho hivyo wananchi waelezwe faida za shirikisho hilo.

Mwanjelwa amewaeleza wabunge kuwa, Wakenya wanaonekana kuwa tishio katika soko la ajira kwa kuwa wameandaliwa, Watanzania hawajaandaliwa, hawajapewa mbinu na mikakati ili wamudu ushindani na kubadili mtazamo wao.

Ametaka Watanzania waelimishwe kwanza mambo muhimu likiwemo suala la soko la pamoja na fedha ya pamoja kabla ya kuingia katika Shirikisho la Kisiasa la EAC, vinginevyo Tanzania itamezwa.