RAIS Jakaya Kikwete amesema, waliotafuna fedha za ruzuku za pembejeo za kilimo watachukuliwa hatua kali za kisheria kwa kuhujumu mpango wa Serikali wa pembejeo hizo kwa wakulima.

Alitoa kauli hiyo alipokuwa akifungua maonesho Nanenane yanayofanyika kitaifa mkoani Dodoma katika Kanda ya Kati eneo la Zunguni nje kidogo ya mji.


Akizungumzia mafanikio ya mradi wa kusambaza pembejeo za kilimo, Rais Kikwete alisema Serikali imetoa fedha kwenye mfuko wa ruzuku kutoka Sh bilioni 7 hadi kufikia Sh bilioni 127 kwa ajili ya ununuzi wa mbegu.


“Serikali imeanzisha mkakati wa kuendeleza sekta ya kilimo na sekta binafsi kwa kuhakikisha kilimo kinakuwa zaidi na nchi inajitosheleza kwa chakula na kuondoa umasikini,” alisema Rais Kikwete.


Alisema Serikali inakusudia kuongeza ajira kwa kuwekeza fedha kwa wanasayansi ambapo tayari wanafunzi 200 wako katika vyuo mbalimbali.


Rais Kikwete alisema Serikali itaendelea kukarabati vituo vya utafiti vya zana za kilimo na vifaa vilivyokuwepo na kuhakikisha mbegu za mazao mbalimbali zinazalishwa kwa kuzingatia ubora kutokana na utafiti.


Aidha Kikwete amesema Serikali ina mpango wa kuanzisha Chuo Kikuu cha Kilimo katika kijiji cha Butiama mkoani mara katika hatua ya kuimarisha sekta ya kilimo nchini na kuongeza upatikanaji wa maofisa ugani ambao watakomboa wakulima.


Pia aalisema serikali itawawezesha maafisa ugani kupata pikipiki ili kuondoa kisingizio kwamba hawawezi kuwafikia wakulima katika maeneo ya mashamba.


Kwa upande wake Waziri wa Kilimo Chakula na Ushirika, Profesa Jumanne Maghembe alisema alisilimia 64 ya wakulima bado wanatumia jembe la mkono nchini na kwamba mpango wa Serikali ni kuwawezesha kupitia vyama vya ushirika ili wawe na zana za kilimo

za kisasa.