Wapiganaji wa Libya wanaendelea kusonga mbele kuelekea mji mkuu, Tripoli.
Televisheni ya wapiganaji hao imewaambia watu wajitayarishe kuwapokea.
Baada ya kuteka eneo la kati ya mji wa Zawiya, magharibi ya Tripoli, wapiganaji sasa wanasema wameiteka bandari muhimu ya Brega, mashariki mwa nchi, yenye kinu cha kusafisha mafuta.
Hakuna taarifa ya kuthibitisha hayo yanayotokea Brega.
Mwandishi wa BBC mjini Zawiya anasema kwenye medani wanayoiita medani ya mashujaa, katikati ya Zawiya, aliona majengo yaliyopigwa mabomu, yanayowaka moto, na kuta zenye matobo ya risasi.

Jana eneo hilo lilidhibitiwa kabisa na jeshi la Kanali Gaddafi.
Kulikuwa na mapigano makali jana jioni hadi usiku.
Lakini wapiganaji sasa wanaudhibiti mtaa, wamewatimua wanajeshi wa Gaddafi ambao wameelekea barabara ya kwenda Tripoli.
Kati ya medani alikuta maiti kama watatu.
Ameona maiti wanaoonesha kama Waafrika, na wapiganaji wanadai kuwa wanajeshi wengi wa Gaddafi ni askari mamluki kutoka kusini ya Sahara.
Ukweli hasa haujulikani, lakini maiti nyingi huko zinaonekana ni za Waafrika.
Sasa wapiganaji wanajitayarisha kusonga mashariki zaidi mwa mji, kuwatimua wanajeshi wa Gaddafi waliobaki Zawiya, ili kufungua njia ya kuelekea Tripoli.
Wapiganaji wa Libya wanadai kuwa waziri mkuu wa zamani, Abdessalem Jalloud, amekimbia Tripioli na amejificha katika maeneo yanayodhibitiwa na wapiganaji.