SERIKALI ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ) imesema washirika wa maendeleo sasa wamefungua milango na kuonesha nia nzuri ya kusaidia maendeleo ya miundombinu ya Kisiwa cha Pemba baada ya kuridhishwa na hali ya kisiasa ya amani na utulivu.

Hayo yalisemwa na Waziri wa Miundombinu na Mawasiliano, Hamad Masoud wakati akitoa salamu za shukrani kwa Serikali ya Marekani mara baada ya kutiwa saini kazi za ujenzi wa barabara tano za Kusini kisiwa cha Pemba huko Wete juzi.

“Nchi washiriki wa maendeleo sasa zinaonekana wazi wazi kwamba zimeridhishwa na mazingira yaliyopo sasa ya amani na utulivu ambayo yamekuja baada ya maridhiano ya kisiasa ya kuwepo kwa Serikali ya umoja wa kitaifa,” alisema Hamad.

Hamad ambaye ni Mwakilishi wa Jimbo la Ole kwa tiketi ya Chama cha Wananchi (CUF) aliishukuru Serikali ya Marekani kupitia mradi wake wa changamoto za milenia (MCA.T) kwa kusaidia kazi za ujenzi wa barabara tano za Pemba ambazo alisema zitasaidia kupunguza umasikini kwa wananchi wa kisiwa hicho.

Mbali ya mradi wa barabara tano za kisiwa cha Pemba, Shirika la Changamoto za Milenia unafadhili mradi wa umeme kutoka Ras-Kilomoni hadi Mtoni.

Jumla ya nchi tano pamoja na mashirika ya kimataifa yanatekeleza miradi mbalimbali ya ujenzi wa barabara za kisiwa cha Pemba ikiwemo Serikali ya Norway pamoja na Benki ya BADEA.