Watu 13 wamepoteza maisha mkoani Singida, kutokana na ajali za barabarani zilizosababishwa na waendesha pikipiki katika kipindi cha kuanzia Januari hadi Juni, mwaka huu.
Mrakibu Msaidizi wa polisi Mkoani Singida, Mohamed Likwapa aliyasema hayo kwenye taarifa ya ajali zilizosababishwa na waendesha pikipiki aliyotoa kwenye hafla ya ufungaji wa mafunzo ya waendesha pikipiki,wa Manispaa ya Singida yaliyofanyika kwenye chuo cha Veta,mjini hapa.
 Aidha, Mrakibu huyo msaidizi alisema katika kipindi hicho ajali za pikipiki zilizotokea ni 48 na kwamba kati ya ajali hizo watu waliofariki walikuwa 13.
Hata hivyo, Likwata ambaye pia ni kamanda wa Kikosi cha Usalama Barabarani Mkoa wa Singida alifafanua kwamba ajali hizo zilisababisha watu 48 kujeruhiwa na kulazwa katika Hospitali mbalimbali kwa ajali ya kupatiwa matibabu.
Kwa mujibu wa Kamanda wa Kikosi cha Usalama Barabarani, ajali nyingi za barabarani zimekuwa zikitokea na kwamba hivi sasa wataanza kuangalia takwimu za matukio ya ajali zitakazosababishwa na waendesha pikipiki hao waliohitimu mafunzo hayo ya wiki mbili.
“Kwa hiyo tutaanza kuangalia takwimu jinsi hawa tuliowafundisha wamewezaje kuzipokea zile taratibu za ufundishaji na kuweza kubadilikaki tabia,”alifafanua Likwata.
Baada ya mafunzo hayo, Kamanda wa Kikosi cha Usalama Barabarani Mkoa aliweka bayana kwamba ni matumaini ya jeshi hilo kuwa waendesha pikipiki hao watabadilika kitabia kutokana na mafunzo waliyopata.
 “Tuna amini kuwa wataweza kubadilika kitabia kwa sababu wao wenyewe wamekubali kabisa kwamba tulikuwa hawajui kabisa sheria za usalama barabarani,”aliweka bayana kamanda huyo.
Kwa mujibu wa kamanda huyo, kuanzia mwezi huu wataendelea kuangalia kasi ya matukio ya ajali za barabarani kadri zitakavyoendelea kutokea kuona kama kuna ongezeko au upungufu ya matukio hayo.
  Akifunga mafunzo hayo,Kamanda wa polisi wa Mkoa wa Singida, Celina Kaluba alisema ajali nyingi za pikipiki zinatokana na uzembe unaosababishwa na waendesha pikipiki ambao idadi kubwa hawazifahamu sheria za usalama barabarani.
  Katika risala ya wahitimu wa mafunzo hayo iliyosomwa na katibu wa umoja huo wa waendesha pikipiki wa Manispaa ya Singida, Maulidi Mpondo aliweka wazi kwamba mafunzo hayo yamewasaidia kufahamu sheria na kanuni za uendeshaji salama barabarani.
 Kwa upande wao, baadhi ya wahitimu wa mafunzo hayo wametumia fursa hiyo kutoa wito kwa waendesha pikipiki wengine wasiopata mafunzo wasisite kujiunga na chuo cha Veta kwa ajili ya kupatiwa mafunzo yatakayowasaidia kufahamu kwa kina sheria za usalama barabarani.
 Mafunzo hayo yaliyotolewa katika Chuo cha Mafunzo ya Ufundi Stadi (VETA) Mkoani Singida,yaliwashirikisha waendesha pikipiki 130 wa Manispaa ya Singida.