WAZIRI wa Katiba na Sheria, Celina Kombani amesema bungeni kuwa, Waziri Kivuli wa Wizara hiyo, Tundu Lissu ni Mchochezi na anawapotosha Watanzania.

Kombani amemtuhumu Lissu kuwa, ana usongo na Urais wa Tanzania, na anavuka mipaka katika baadhi ya mambo anayozungumza.

Waziri Kombani amemtuhumu Lissu kwamba amewasilisha bungeni Muswada wa Mabadiliko ya Katiba bila idhini yake, na amemuuliza Spika wa Bunge kama Kanuni za Bunge zinaruhusu mawaziri vivuli kufanya hivyo.

“Avute subira, asubiri wakati wa kuchangia Katiba yake yote ya tumboni yatatoka” amesema Kombani wakati anajibu hoja za wabunge waliochangia bajeti ya Wizara hiyo kwa mwaka wa fedha 2011/2012.



“Hatujaanza kujadili Katiba mpya, wakati haujafika” amesema Kombani na kusisitiza kwamba, Katiba si lelemama, ni sheria mama.

Kombani amewaeleza wabunge kuwa, anaona dalili ya watu wachache wanaotaka kuhodhi Katiba mpya. Ameonya kuwa, kama suala la Katiba likifanywa ni la kisiasa Taifa halitafika mbali.

Kombani amesema, hana uhakika kama aliyoyasema Lissu kwenye hotuba ya kambi ya upinzani ni maoni ya kambi hiyo au ni mawazo yake binafsi na amemshauri Mbunge huyo awe mwangalifu anapozungumza kama walivyo majaji.

Amesema, hana uhakika kama kambi ya upinzani ilipata fursa ya kuipitia hotuba aliyoisoma Lissu bungeni, na kama ingekuwa hivyo wasingemruhusu aisome.

“Upande wa Upinzani muwe mnapitia hizo hotuba kabla” amesema Kombani na kwamba, wasipofanya hivyo mtu anaweza kusoma madudu yake bungeni.

Waziri Kombani amesema, Mungu amempa kila mtu karama, hivyo ‘tuzitumie vizuri hizo karama zetu”.

Amesema,yeye (Kombani) amefundishwa protokali, na ni Ofisa Utumishi, hivyo haelewi kama Lissu alitaka yeye (Kombani) aende barabarani au alie kwa sababu bajeti ya Wizara haitoshi.

Waziri Kombani amewaeleza wabunge kuwa, Lissu ametoa tuhuma nzito kuhusu ufisadi katika idara ya Mahakama, na amemtaka Waziri huyo kivuli wa Katiba na Sheria awe anahudhuria vikao vya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Katiba, Sheria na Utawala ili azipate vizuri taarifa za Serikali.