Waziri mkuu wa uturuki Recep Tayyip Erdogan anatarajiwa kuwasili nchini Somalia kuanzisha rasmi kampeni ya kukabiliana na baa la njaa nchini humo.
Waziri huyo mkuu ataandamana na waziri wake wa mashauri ya nchi za kigeni na wake zao. Viongozi hao wamesema wako nchini Somalia kuonyesha wanawaunga mkono raia wa Somalia.Bendera za uturuki zimekuwa zikipaa katika uwanja wa ndege na bandari kuu mjini Mogadishu ikiwa ni ishara kuwa mji huo upo tayari kumpokea waziri mkuu Erdogan.
Ziara yake hii huenda ikawa na malengo mawili.
Moja ni kushuhudia harakati za kusamabaza misaada iliochangwa na raia wa nchi yake.
Pia kiongozi huyo na msafara wake wa mawaziri na wake zao pia unahamu kujionea wenyewe matatizo yanayo wakabili raia wa somalia.
Kando na misaada ya vyakula na madawa, raia wa uturuki wamechanga kiasi cha dola 115 milioni kusaidia walioathirika na njaa nchini humo.
Serikali ya uturuki pia inalenga sana kuongeza ushawishi wake barani Afrika.
Kando na mchango wake kibiashara, utawala huo unathamini bara hili ambalo kwa kiasi kikubwa kura zake zilisaidia nchi hii kupata nafasi ilionayo kwenye baraza la usalama la umoja wa mataifa.
Ikiwa waziri mkuu Erdogan atafaulu kuchangia kwa kiasi kikubwa kwenye mikakati ya kutatua mzozo unaoendelea nchini Somalia basi hii itakuwa njia moja ya nchi yake kupewa heshima barani humu na kwenye ngazi za kimataifa.
0 Comments